Jumatano , 16th Jun , 2021

Baaada ya mchezo wa kwanza wa kundi D wa Portugal 3-0 Hungary kumalizika saa tatu usiku wa jana na CR7 kucheza dakika zote 90 na kufunga mabao 2, nyota huyo ameendelea kuweka rekodi kibao na kumfanya aibuke na tuzo ya mchezaji nyota wa mchezo huo.

Nyota wa timu ya taifa ya Ureno, Cristiano Ronaldo 'CR7'.

Rekodi alizoziweka Ronaldo ni pamoja na:

CR7 amefikisha mabao 11  na kumpiku mwamba wa Ufaransa, Michael Platini aliyekuwa na mabao 9 hivyo kumfanya CR7 kuwa mchezaji pekee mwenye mabao mengi tokea kuanzishwa kwa michuano ya UEFA EUROS miaka 60 iliyopita. Mfungaji bora wa muda wote. 

CR7 ndiye mchezaji pekee kucheza michuano ya UEFA EUROS kwa awamu 5 (2004, 2008, 2012, 2016 na mwaka huu 2021) na kumpiku Lothar Matthaus wa Ujerumani aliyecheza EUROS awamu 4 (1980, 1984, 1988 na 2000).

CR7 ndiye mchezaji pekee kucheza michezo mingi, michezo 22 kwenye michuano ya UEFA EUROS na kuvunja rekodi aliyekuwa anaishikilia kiungo chuma wa zamani wa timu ya taifa ya Ujerumani, Bastian Shweinsteiger aliyekuwa amecheza michezo 21. 

CR7 amefikisha jumla ya mabao 105 mabao 4 nyuma ya Ali Daei wa timu ya taifa ya Iran ambaye anaongoza kuwa mfungaji bora wa muda wote kwa upande wa timu za taifa, rekodi ambayo anazidi kuifukuzia.

Baada ya rekodi hizo, Ureno sasa ni kinara wa kundi D akiwa na alama 3 na mabao 3, Ufaransa anashika nafasi ya pili akiwa na alama 3 lakini na bao 1 baada ya kumfunga ujerumani 1-0 hivyo Ureno anaongoza kwa utofauti wa mabao ya kufunga huku Ujerumani akishika nafasi ya tatu na Hungary akishika mkia.

Michuano hiyo inatazamiwa kuendelea tena usiku wa leo Juni 16, 2021 kunako kundi F, wanaoshika mkia kundi hilo, Uturuki itacheza na Wales waliopo nafasi ya tatu saa 1:00 usiku na kinara, Italia itacheza na Uswizi anayeshika nafasi ya pili saa 4:00 usiku.