Jumamosi , 15th Feb , 2025

Chama cha ACT Wazalendo wamepinga vikali kauli iliyotolewa jana Februari 14, 2025 na Waziri wa Ujenzi, Ndg. Abdallah Ulega, akipendekeza kuwekwa utaratibu wa kulipia matumizi ya barabara ya mwendokasi kwa wale wanaotaka kuepuka foleni.

Chama cha ACT Wazalendo wamepinga vikali kauli iliyotolewa jana Februari 14, 2025 na Waziri wa Ujenzi, Ndg. Abdallah Ulega, akipendekeza kuwekwa utaratibu wa kulipia matumizi ya barabara ya mwendokasi kwa wale wanaotaka kuepuka foleni.

 

Chama hicho kimebainisha kuwa kauli ya Waziri Ulega haipaswi kupuuzwa na kuwa ni ushahidi mwingine wa jinsi serikali inavyokosa huruma kwa wananchi wake na kukosa uwajibikaji kwa maslahi ya wananchi.

 

ACT wamesisitiza mradi wa mabasi ya mwendokasi jijini Dar es Salaam ulijengwa kwa fedha za walipa kodi wa Tanzania na hivyo ni haki ya kila mwananchi kuutumia bila vikwazo vya gharama.

 

Hivyo kuweka ada kwa huduma ambayo ilikusudiwa kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri wa umma ni kinyume na malengo na kuwa ni ubaguzi wa wazi ambapo wananchi maskini watalazimika kubaki kwenye foleni kwa sababu hawawezi kumudu gharama mpya.

 

Taarifa ya chama hicho imeenda mbali zaidi kwa kusisitiza kuwa mfano uliotolewa na Waziri Ulega kuhusu Daraja la Mwalimu Nyerere Kigamboni kama jambo la mafanikio ni dhihaka kwa wananchi na linashangaza, kwani licha ya malalamiko ya muda mrefu kuhusu ada kubwa za daraja hilo na serikali kutoonesha nia ya kushughulikia changamoto hiyo, Waziri amependekeza mfumo huo waliouita ni "wa uonevu" uendelezwe kwenye barabara za mwendokasi. Huu ni uthibitisho kwamba serikali ya CCM haina ajenda ya maendeleo yanayowalenga wananchi bali inaendeleza siasa za kutengeneza vikwazo vya kiuchumi kwa wananchi.

 

 

ACT wameitaka serikali kuacha mara moja mawazo hayo "dhalimu" na badala yake kuelekeza juhudi katika kuboresha miundombinu kwa ajili ya wote pia wametoa wito kwa Serikali kutafakari ujenzi wa barabara za mzunguko (ring roads) kuzunguka Mji wa Dar es Salaam ili kuyaondoa Malori kutumia barabara za katikati ya mji yanapobeba mizigo kutoka bandari ya Dar e s Salaam.