Ijumaa , 8th Jul , 2016

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu UNFPA, limesema asilimia 27 ya wanafunzi wa kike nchini wanapata ujauzito kabla ya kuhitimu elimu ya shule ya msingi nchini Tanzania

Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya watu UNFPA, limesema asilimia 27 ya wanafunzi wa kike nchini wanapata ujauzito kabla ya kuhitimu elimu ya shule ya msingi nchini Tanzania kutokana na mazingira duni ya kielimu wanayokabiliana nayo katika maeneo ya vijijini.

Shirika hilo likielekea kuadhimisha Siku ya Idadi ya watu hapo Julai Mosi, Mratibu Mkazi wa UNFPA nchini Tanzania, Dkt. Natalia Kanem amesema kuna umuhimu wa kuwekeza zaidi katika elimu kwa vijana ikiwa ni pamoja na elimu ya afya ya uzazi kutokana na matokeo ya utafiti kuonesha hali ni mbaya zaidi ikilinganisha na miaka mitano iliyopita

Akizungumzia kuongezeka kwa Idadi hiyo ya watoto wanaoacha shule za Msingi Nchini Tanzania kufuatia mimba za utotoni, Mratibu Mipango wa Shirika hilo, Samwel Msokwa amesema asilimia 42 ya wasichana wameanza kuwa wazazi wakiwa hawajahitimu elimu ya msingi nchini.

Kwa Upande wao Afisa Mipango wa Ukimwi na VVU Dkt. Majaliwa Marwa na Afisa Mipango wa afya ya uzazi kwa vijana kutoka UNFPA Fatna Kiluvia wanasema vijana wengi hawana elimu ya kutosha ya afya ya uzazi ikiwa ni pamoja na namna ya kujikinga na maambukizi ya mapya ya Virusi ya Ukimwi na hivyo kuwa waathirika wakubwa.