Jumanne , 10th Jul , 2018

Ikiwa ni siku chache toka Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Paul Makonda kusitisha zoezi la kufunga maduka hadi saa 4:00 asubuhi siku za Jumamosi wafanyabishara na wananchi wamesema kuwa tabia hiyo ilijenga uadui kati ya wafanyabiashara na serikali.

Pichani wananchi wakifanya usafi.

Akizungumza na eatv.tv mmoja kati ya wafanyabiashara, Eliud Mfweya ambaye anauza duka maeneo ya Sinza amesema kuwa zoezi hilo lilikuwa likiathiri biashara zao pamoja na kushusha uchumi.

Usafi uligeuka uadui baina ya sisi wauza maduka na serikali maana hatukutakiwa kukutwa tumefungua maduka kabla ya muda huo na wakati huo huo sio wote waliokuwa wakifanya usafi, bora huu utaratibu mtu atafanya usafi kwa muda wake na akikutwa eneo chafu atatozwa faini, huku biashara zikiendelea”, amesema Mfweya.

Naye Juma Ramadhani amesema kuwa sheria ya kufunga maduka asubuhi siku za Jumamosi ilikuwa kero kwani unaweza kuwa na shida ya haraka lakini ukashindwa kutimiza kwa wakati kutokana na maduka kufungwa.

Makonda alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Vijana wa JKT na Mgambo, waliojitokeza katika usaili wa kuajiriwa ili kusimamia zoezi la usafi na kuhakikisha wanawawajibisha wanaochafua mazingira jijini, huku wafanyabiashara wakifungua maduka yao kama kawaida.