Jumatano , 28th Aug , 2019

Uongozi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, umekanusha taarifa zilizoenea katika mitandao ya kijamii juu ya matokeo ya mitihani ya wanafunzi chuoni hapo, inayodai kuwa takribani  wanafunzi 1129 wamefeli 'disco' kuendelea na masomo huku wengine zaidi ya 7000 wakitakiwa kurudia mitihani.

Jengo la kitivo cha biashara, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam

Akizungumza na EATV & EA Radio Digital leo Agosti 28, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayehusika na taaluma, Profesa Boniventura Rutina amesema taarifa hizo si za kweli  na kwamba hata kikao cha seneti kinachopitisha matokeo hayo bado hakijakaa.

''Na mimi taarifa hizo kwenye mitandao niliziona, taarifa hizo ni za uzushi kwa sababu matokeo ya chuo hutolewa na seneti na seneti inakaa tarehe 30 Ijumaa, sasa wenyewe wamepata wapi matokeo ambayo hayajatolewa?, matokeo bado hilo ndio jibu'', amesema Profesa Rutina.

Aidha Profesa Rutina amewatoa hofu wanafunzi, wazazi pamoja na wananchi na kuwahakikishia kwamba chuo hicho kitaendelea kusimamia taaluma, ubora, ubunifu uwajibikaji na maaadili kwa wanafunzi na wafanyakazi wake.