TRA kutoza Mil. 1.5 kwa watakayemkuta hana risiti 

Alhamisi , 7th Jan , 2021

Mamlaka ya Mapato Nchini (TRA), imesema kuwa wataanza msako katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la kuwakagua na kuwatoza faini wanunuaji wanaonunua bidhaa bila kuomba risiti na wafanyabiashara wanaouza bidhaa bila kutoa risiti.

Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka TRA, Richard Kayombo

Kauli hiyo imetolewa hii leo Januari 7, 2021, na Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Mlipa Kodi kutoka TRA, Richard Kayombo, wakati akizungumza kwenye kipindi cha SupaBreakfast cha East Africa Radio.

"Kama hautachukua risiti kwenye huduma ama bidhaaa yoyote uliyonunua ambayo inatakiwa kutolewa risiti, unaweza ukatozwa faini ya shilingi 30,000 au Milioni 1.5", amesema Kayombo.

Aidha akizungumzia kuhusu wafanyabiashara wasiokuwa waaminifu, Kayombo amesema kuwa, "Kama umeuza bidhaa lakini hujatoa risiti adhabu yako ni kati ya Mil. 3 hadi Mil. 4.5 iwe umetoa risiti ya udanganyifu adhabu hiyo inakuhusu au unayo mashine lakini hauitumii".