Alhamisi , 6th Sep , 2018

Mfanyabiashara raia wa China anayeishi nchini Kenya, Liu Jiaqi amekamatwa na serikali ya Kenya kufuatia kusambaa kwa video yake katika mitandao ya kijamii inayomuonesha akiwakashifu raia pamoja na Rais wa nchi hiyo, Uhuru Kenyatta.

"Kibali chake cha kazi kimefutwa na atafukuzwa nchini kutokana na ubaguzi", imesema taarifa ya mamlaka ya Uhamiaji ya nchi hiyo katika mtandao wa twitter.

Video hiyo iliyosambaa katika katika mitandao ya kijamii inamuonesha mfanyabiashara huyo akirekodiwa na mfanyakazi wake huku akisema,

"Kila mmoja, kila mkenya ni kama nyani, akiwamo Uhuru Kenyatta, hao wote", amesema katika video hiyo.

Aliposhauriwa na mfanyakazi huyo kuwa arejee kwao China endapo hapendi kuendelea kuishi Kenya, alijibu,

"Mimi si mkazi wa hapa, sipapendi hapa, watu wake ni kama nyani na sipendi kuongea nao, pananuka harufu mbaya, masikini na watu ni weusi, siwapendi. Kwanini hawako kama watu weupe, kama wamarekani ?", ameongeza mfanyabishara huyo huku akisema kinachomfanya aendelee kuishi Kenya ni kwaajili ya fedha.

Kwa mujibu wa msemaji wa ubalozi wa China nchini Kenya, Zhang Gang, video hiyo ilirekodiwa mwezi Juni na tayari alishachukuliwa hatua na kampuni yake kwa kitendo hicho huku akiwaomba radhi wakenya kwa tukio hilo.

Hiyo sio mara ya kwanza kwa raia wa China kutuhumiwa kwa ubaguzi, miaka mitatu iliyopita mgahawa mmoja wa kichina ulifungwa na mamlaka ya mji wa Nairobi na mmiliki wake kutozwa faini baada ya kuanzisha utaratibu wa kuwazuia watu weusi kuingia kuanzia saa 5 usiku.