Ijumaa , 29th Apr , 2022

Madini yenye thamani ya Shilingi trilioni 6.439 yalizalishwa na kuuzwa nchini katika kipindi cha Julai 2021 hadi Machi 22, 2022, hii ni kwa mujibu wa ripoti ya Waziri wa Madini Dkt. Dotto Biteko wakati akiwasilisha mapendekezo ya Bajeti ya wizara mwaka wa fedha 2022/2023 Bungeni, Dodoma.

Pichani ni dhahabu, madini yanayochimbwa Tanzania

Waziri wa madini Dkt. Dotto Biteko ambaye pia ni mbunge wa jimbo la Bukombe mkoani Geita, amesema kuwa katika kipindi cha Mwezi Julai 2021 na Machi, 2022, shilingi bilioni 429.19 zilikusanywa kama malipo ya mrabaha na ada ya ukaguzi kutoka kwenye madini mbalimbali yaliyochimbwa nchini Tanzania.

Katika mchanganuo wake, kulirekodiwa Kilogramu 39,682.94 za dhahabu, karati 155,117.10 za almasi, Kilogramu 15,377.44 za Tanzanite ghafi, na Tani 956,688.08 za makaa ya mawe miongoni mwa aina nyingine za madini yaliyopo nchini.

Hata hivyo, Waziri Biteko amefafanua kwamba, makusanyo hayo ni ongezeko la asilimia 2.5 ikilinganishwa na Sh bilioni 418.7 zilizokusanywa katika kipindi kama hicho kwa mwaka 2020/2021.

Aidha, Waziri Biteko amesema changamoto ya vita kati ya Urusi na Ukraine inaweza kuchochea mahitaji makubwa ya madini ya dhahabu ulimwenguni na kuongeza kwamba Uchumi wa madini nchini kwa kiasi kikubwa unatokana na madini ya dhahabu, ambayo huchangia takribani asilimia 80 ya mapato yatokanayo na rasilimali madini.