Jumatano , 21st Sep , 2022

Baadhi ya wafanyabiashara na walaji wa kuku wa kisasa Katika Jiji la Dar es Salaam wamelalamikia kuadimika kwa kitowewo hicho, huku wengine wakiuza ambavyo havijakomaa.

Kuku wakiwa katika soko la Mwananyamala

EA Radio ilibaini kuwapo kwa uhaba huo baada ya kutembelea masoko mbalimbali ambayo wafanyabiashara walikuwa wanauza kuku wadogo wanaokadiriwa kuwa chini ya miezi sita.

Katika soko la Mwananyamala,  wafanyabiashara wengi wameonekana wakisubiri magari yanayoleta kuku bila mafanikio, huku wafanyabiashara wa kuku wakisema hata wanaopatikana ni kuku wadogo na kwamba hawakidhi mahitaji ya soko na wateja.

Aidha, EA Radio iliwaona wafanyabiashara wa chipsi na mama lishe katika masoko ya Mwananyamala na Shekilango wakiondoka sokoni bila kitoweo hicho, huku Mbaraka Said Salum, Mwenyekiti wa soko la Mwananyamala akisema kuwa sababu ya hali hiyo ni kupungua kwa uzalishaji wa kuku kwakuwa wazalishaji wa vifaranga wamepungua na athari za baridi pia.