Jumanne , 13th Sep , 2022

Soko la Hisa la DSM (DSE) limeshuhudia ongezeko la ukwasi kwa asilimia 10 kwa upande hisa kutoka Shilingi Bilioni 7.46 hadi Shilingi Bilioni 8.22 katika kipindi cha wiki moja iliyopita, kiwango kinachotajwa kimetokana na kuongezeka kwa wawekezaji wa nje.

Leonard Kameta, Meneja uendelezaji biashara DSE

Meneja Maendeleo ya Biashara wa Soko hilo Leonard Kameta amewaambia waandishi wa habari jijini DSM kuwa, mauzo yaliyofanyika katika kaunta za NMB yalichangia ukwasi huo kwa asilimia 82.32 sawa na Shilingi Bilioni 6.8, CRDB asilimia 12.66 sawa na Shilingi Bilioni 1.04 na Kampuni ya Sigara TCC iliyochangia kwa asilimia 2.50 sawa na Shilingi Milioni 206.

Hata hivyo katika kipindi hicho kilichoishia Septemba 9 mwaka huu, ukubwa wa soko la ndani (Domestic Market Capitalization) ulipungua kwa kiwango cha Asilimia 0.1 kutoka Shilingi Trilioni 10.35 hadi Shilingi Trilioni 10.34, sababu kubwa ikitajwa kupungua bei za kampuni za Mwalimu, Swiss Sport na CRDB.

Kwa upande wa hatifungani, thamani iliyoorodheshwa DSE imeongezeka kwa Shilingi 0.01 Trilioni kutoka Shilingi Trilioni 16.10 hadi kufikia Shilingi Trilioni 16.11 kutokana na kuongezeka kwa mauzo ya hatifungani za serikali.