Wednesday , 6th May , 2015

Serikali imesema itawazawadia wanafunzi, walimu pamoja na shule zilizofanya vizuri ikiwa ni motisha katika sekta ya elimu katika maandhimisho ya wiki ya elimu ambayo yataanza tarehe 11 na kuhitimishwa tarerehe 15 mwezi wa 5 mwaka huu.

Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa.

Akizungumza na East Africa Radio leo Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa amesema lengo kuu la maadhimisho hayo ni kuangalia changamoto na mafanikio yaliyopatikana kupitia mpango wa Matokeo Makubwa sasa BRN katika sekta ya Elimu.

Dkt. Kawambwa amesema changamoto kubwa katika sekta hiyo ni madawati na vitabu ambapo serikali imejitahidi kulitatua suala hilo kupita chenji ya rada pamoja na misaada ya taasisi mbalimbali na kuongeza kuwa serikali imetenga fedha kwa ajili ya kulimaliza kabisa tatizo hilo.

Aidha Waziri huyo ameongeza kuwa katika upande wa shule wa sekondari kwenye masomo ya sayansi wamepiga hatua ambapo kwa sasa wanakaribia kufikia kitabu kimoja kwa mwanafunzi mmoja.

Pia amesema kwa serikali ina mpango wa kuboresha miundombinu kwa shule za wananchi ikiwa ni maabara, madarasa pamoja na nyumba za walimu katika mpango wa maendeleo wa shule za sekondari awamu ya pili MMES II