Saturday , 25th Apr , 2015

Zaidi ya wachezaji ishirini wa mchezo wa Darts toka maeneo mbalimbali hapa nchini hii leo wamechuana vikali katika siku ya kwanza ya michuano ya taifa ya mchezo wa darts ambayo imeanza hapa jijini Dar es Salaam

Baadhi ya wachezaji wa mchezo wa darts wakichuana jijini Dar es Salaam.

Mashindano ya taifa ya siku mbili ya mchezo wa vishale [darts] ya singles na doubles yameanza hii leo katika ukumbi wa Moshi Hotel jijini Dar es salaam na kuhudhuriwa na wachezaji mbalimbali toka mikoa mitano wanachama wa chama cha darts Tanzania TADA

Katibu mkuu wa chama cha darts Tanzania TADA Kale Mgonja amesema wamefarijika na mwitikio mkubwa wa wachezaji wengi hasa kuongezeka kwa wachezaji wanawake katika mashindano hayo ambayo mara hii yanafanyika kwa mwaka wa tatu sasa tangu kuanzishwa kwake miaka mitatu iliyopita

Kale amesema kati ya mikoa wanachama hai tisa wa chama cha Darts Tanzania TADA ni mikoa mitano pekee ndiyo iliyoshiriki ambayo ni Arusha, Morogoro, Mbeya, Dodoma na wenyeji Dar es Salaam ambao wachezaji wake watakaofanya vema katika mchuano huo wataliwakilisha taifa katika michuano mikubwa ya kimataifa kwa nchi za Afrika Mashariki na kati itakayofanyika mwezi Juni mwaka huu jijini Kampala nchini Uganda.

Aidha Kale amesema mikoa mingine minne wanachama wa TADA ya Kilimanjaro, Mara, Kagera na Mwanza haikuja kushiriki kutokana na mikoa hiyo kukumbwa na ukata wa fedha lakini wao kama chama watajipanga msimu ujao kutafuta wadhamini wakutosha ili kuzisaidia timu ama mikoa na wachezaji binafsi kuwapunguzia gharama ili waweze kushiriki michuano mbalimbali ijayo.