Friday , 1st May , 2026

Meneja wa Habari wa klabu ya Simba, Ahmed Ally amethitibitisha kuwa wachezaji watatu wa klabu hiyo Anicet Oura, Nickson Kibabage na Yusuph Kagoma ambao walitolewa kwenye fainali ya Kombe la Muungano 2026 dhidi ya Yanga SC wapo vizuri kuelekea Dabi ya Mei 3, 2026 kwenye ligi kuu bara.

Anicet Oura

"Napenda kuwajulisha kwamba wachezaji wote (Oura, Kibabage na Kagoma) ambao walitolewa katika mchezo wa fainali ya Kombe la Muungano kwa kuumia, wote wako tayari kwa mchezo wa Jumapili. Ninapozungumza hapa wachezaji wapo vizuri kabisa, cha kufanya ni kumuomba Mwenyezi Mungu aendelee kulinda hali zao.”

“Kama sisi tutashindwa kupunguza gap libaki alama mbili, tusitegemee Singida au timu zingine ndio zitawazuia. Adui unayemuweza mmalize wewe mwenyewe, tusitegemee hao wengine kuja kumpurutisha alama nane. Wanasema mtegemea cha ndugu hufa masikini.”

“Msimu huu tumedhamiria kurejesha heshima yetu. Msimu huu hatupo tayari kumaliza patupu, watakachokipata tutakipata, watakachokikosa tutakipata. Tumeanzia Zanzibar wao wamechukua Mapinduzi, sisi Muungano. Tumehamia Ligi Kuu na Kombe la Shirikisho, either tuchukue yote au tugawane na timu ya kuchukua makombe yote tunayo. Msimu huu ni kupata furaha kamili au tugawane.”

“Msimu huu tumekutana mara tatu, wametufunga moja, tumewafunga mara mbili. Na mechi ambayo ilionekana ni sare mwamuzi alishushwa daraja, taarifa ya Bodi ya Ligi ilisema lilikuwa goli halali.”