Monday , 29th Dec , 2025

Kuanzishwa kwa safari za ziada ni hatua ya kupunguza usumbufu uliowakumba abiria na kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.

Kutokana na usumbufu uliojitokeza kwa abiria jana Desemba 28, 2025, Shirika la Reli Tanzania (TRC) limeanzisha safari za ziada za Treni ya Reli ya Kisasa (SGR) kwa lengo la kuwahudumia abiria hao.

Akizungumza kupitia taarifa iliyotolewa kwa umma leo, Desemba 29, 2025, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano kwa Umma wa TRC, Fredy Mwanjala, amesema kuanzishwa kwa safari za ziada ni hatua ya kupunguza usumbufu uliowakumba abiria na kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.

Hatua hiyo imechukuliwa kufuatia maelezo ya Wizara ya Uchukuzi kuwa mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini zimesababisha athari katika miundombinu ya SGR na barabara, hali iliyoathiri ratiba za usafiri na kutishia usalama wa wasafiri.

Taarifa ya wizara hiyo kwa umma ilitolewa jana wakati huduma za SGR tayari zilikuwa zimeathirika, baada ya baadhi ya abiria kushindwa kuanza safari zao kwa mujibu wa ratiba.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, treni iliyopaswa kuondoka saa 12:00 asubuhi ilikwama katika Stesheni ya Magufuli jijini Dar es Salaam, na hadi saa 6:24 mchana haikuwa bado imeanza safari.