Wednesday , 30th Jul , 2025

Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 8.8 katika kipimo cha Richter limeripotiwa mapema Jumatano katika pwani ya mashariki mwa Urusi na hivyo kuchochea tahadhari ya tsunami huko Japan, Alaska, Peru na Hawaii.

Kwa mujibu wa Mamlaka ya Jiolojia ya Urusi, tetemeko hilo ni kubwa kabisa kuwahi kulipiga eneo hilo la Rasi ya Kamchatka tangu mwaka 1952.

Tsunami  iliyosababisha mawimbi makubwa ya bahari imeripotiwa katika visiwa vya Hokkaido vya Japan na visiwa vya Kuril vinavyomilikiwa na Urusi, na yanahofiwa kuelekea pia Ufilipino, Chile na Visiwa vya Solomon.

Tayari mataifa kadhaa katika pwani ya  Bahari ya Pasifiki  kama vile Ufilipino, Colombia na mengineyo yametangaza tahadhari ya kiwango cha juu ya kutokea Tsunami.

Athari za tetemeko hilo zinatazamiwa kuonekana hadi nchini Marekani kwenye miji ya Carlifornia na Washington.
Uwanja wa ndege wa Kahului unaopatikana katika kisiwa kikubwa cha Hawaii cha Maui, umefuta safari zote za ndege kutokana na kitisho kilichosababishwa na tsunami.

Ripoti zinasema jimbo la Alaska pia limeathiriwa na tsunami. Juhudi za kuwahamisha wakazi katika maeneo salama zinaendelea kote katika eneo la Pasifiki, huku tahahari ya tsunami ikitolewa nchini Peru na nchi jirani ya Chile.