Thursday , 10th Jul , 2025

Katibu Mkuu wa Chama Cha Makini Taifa, Ameir Hassan Ameir, amesema kuwa endapo wananchi wa Zanzibar watampa ridhaa ya kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi katika uchaguzi ujao, atahakikisha kila mwananchi wa Zanzibar anapokea mshahara wa shilingi 500,000 za Kitanzania

Ameir ametoa kauli hiyo leo katika kikao kazi kilichofanyika kwenye Ukumbi wa Idara ya Habari (Maelezo) Zanzibar, kilicholenga kujadili utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020-2025 pamoja na matarajio ya ilani ijayo ya mwaka 2025-2030.

Akizungumzia mpango huo, Ameir amesema lengo ni kupunguza kwa kiasi kikubwa changamoto za umasikini, ukosefu wa ajira na utegemezi miongoni mwa wananchi wa Zanzibar, hasa vijana na wanawake.

"Tunahitaji mapinduzi ya kweli ya kiuchumi, ambayo yanamwezesha kila Mzanzibari kunufaika moja kwa moja na rasilimali za nchi yake. Serikali yangu itahakikisha kila mwananchi anakuwa na kipato cha uhakika kila mwezi, kupitia mshahara wa TZS 500,000,” alisema.

Aidha, alibainisha kuwa fedha hizo zitatokana na uboreshaji wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, uwekezaji wa kimkakati katika sekta ya utalii, mafuta na gesi, pamoja na kudhibiti matumizi yasiyo ya lazima ya serikali.

Katika kikao hicho, Ameir pia amezipongeza Jitihada za Utekelezajinwa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi Ccm iliyotekelezwa na Raisi wa Zanzibaar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Ali Mwinyi,Kwa Utekelezaji wa Miradi ya kimaendeleo.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, wanaharakati, waandishi wa habari na Viongozi wa Dini, walioonesha shauku ya kutaka kujua mustakabali wa kisiasa na kiuchumi wa Zanzibar kuelekea uchaguzi mkuu wa 2025.