Daniel Maldini ameweka rekodi ya kuwa Mwanaukoo wa tatu kutoka Familia ya Wacheza Soka nchini Italia baada ya jana Oktoba 14, 2024 kwenye mchezo wa ligi ya Mataifa ya Ulaya dhidi ya timu ya Taifa ya Israel Daniel amefuata nyayo za Babu yake Cesare Maldini na Baba yake Paulo Maldini wote kuitumikia The Azzurri kwa vizazi vitatu tofauti.Cesare alianza kuitumikia Italia 1960,Paulo 1988 na Daniel 2024.
Timu ya Taifa ya Italia jana usiku Oktoba 14ilicheza mchezo wa ligi ya mataifa ya Ulaya dhidi ya nchi ya Isreal na kushinda kwa ushindi wa goli 4-1. Kivutio kikubwa katika mchezo huo kilikua ni kitendo cha Daniel Maldini kuingia uwanjani kuitumikia Italia kwa mara kwanza tangu aanze kucheza soka.
Ukoo wa Maldini unaheshimika nchini kwao sababu umetoa Wachezaji waliotengeneza heshima kubwa kipindi chote cha uchezaji wao katika timu ya Taifa na klabu yao ya AC Milan. Babu yake Cesare Maldini alianza kuitumikia timu ya Azzurri mwaka 1960, Baba yake Paulo Maldini 1988 na Daniel Maldini mechi yake ya kwanza timu ya Taifa kubwa ya Italia ilikua siku ya jana Oktoba 14, 2024.
Cesare Maldini, Paulo Maldini na Daniel Maldini pia wameweka rekodi ya kuiwakilisha timu ya AC Milan kwa vipindi tofauti. Paulo Maldini ndiye alikuwa maarufu na aliyefanikiwa zaidi kati ya wote alifanya vizuri akiwa na jezi ya Rossoneri alishinda ubingwa ligi kuu nchini Italia Escudeto mara 7, ubingwa ligi ya mabingwa barani Ulaya mara 5 sambamba na makombe mengine ya ndani Italia.
Daniel Maldini amepita kwenye njia zote alizopita Baba yake kuanzia timu ya Watoto ya AC Milan na Italia. Nyota huyo ambaye kwa sasa anaitumikia timu ya Monza ya inayoshiriki Serie A anacheza eneo la kiungo wa ushambuliaji au eneo la ushambuliaji wa kati kwenye klabu yake na timu ya Taifa ya Italia.
Mjukuu wa Mzee Cesare Maldini kwa Mtoto wake Paulo Maldini alizaliwa Oktoba 11, 2001 kwa sasa ana umri wa miaka 23. Anatakiwa kuandika historia yake binafsi asiangalie jina na historia ya Baba yake aliyoiweka kipindi anacheza mpira.
Watoto wengi wa Wachezaji wa mpira ambao Baba zao walifanikiwa na waliimbwa sana Duniani enzi za uchezaji wao wameshindwa kufanikiwa kwenye safari yao ya mpira na kujikuta wakistaafu wakiwa bado na umri mdogo mfano mzuri Mtoto wa Zinedine Zidane, Enzo Zidane.