Nahodha wa Ureno Criastiano Ronaldo amefunga goli lake la 133 akiwa na jezi ya timu ya Taifa lake kwenye mchezo waliocheza ugenini dhidi ya Poland siku ya jana Oktoba 12, 2024, kumfanya aendelee kuiweka vizuri rekodi yake ya kuwa Mchezaji aliyefunga goli nyingi kwenye michezo rasmi ya kimataifa kwa upande wa Wanaume. Kwenye ushindi dhidi ya Poland Ronaldo amefikisha goli la 903 tangu aanze kucheza soka.
Cristiano Ronaldo ameifungia goli moja timu yake ya Taifa ya Ureno kwenye mchezo wa Mataifa ya Ulaya ugenini dhidi ya Poland katika ushindi wa goli 3-1, Ronaldo alifunga goli la pili baada ya kazi nzuri iliyofanywa na Rafael Leao.
Goli hilo linamfanya Ronaldo mwenye umri wa miaka 39 kufikisha goli lake la 133 akiwa na jezi ya Taifa lake na kuendelea kutanua wigo wa idadi ya goli nyingi kwenye timu za Taifa na kuwaacha mbali Lionel Messi mwenye goli 109 na Ali Daei wa Iran aliyefunga goli 108.
Nahodha huyo wa Ureno ameweka wazi kuhusiana na kustaafu kucheza soka amesema hafikirii kutundika daruga kwa sasa maana bado ananguvu na hamasa ya kuendelea kucheza. Mchezaji bora wa Dunia mara tano anapambania rekodi ya kufunga goli 1000 ili awe Mchezaji pekee Ulimwenguni kufikisha idadi hiyo ya magoli.
Roberto Martinez raia wa Hispania ambaye ndiye Kocha Mkuu wa Mabingwa wa kombe la Mataifa ya Ulaya mwaka 2016, ameweka wazi nia yake ya kuendelea kumtumia Ronaldo kama Nahodha wake kutokana na takwimu zake kwenye kikosi chake.
Mpaka sasa Mchezaji huyo wa zamani wa Sporting Lisbon, Manchester United, Juventus Turin anaitumikia timu ya Al Naseer nchini Saudi Arabia ameendelea kuwa Mchezaji muhimu wa kikosi hiko hivyo kuweka uwezekano wa kufikisha goli 1000 katika maisha yake ya soka kuwa ni ndoto anayoweza kuitimiza.
Ronaldo ndiye nyota bora zaidi kuwahi kutokea nchini Ureno mbele ya Eusebio, Manuel Rui Costa, Paul Futre na Luis Figo.
Nyota huyo aliyewahi kutwaa Ballon D'or mwaka 2008 akiwa na Manchester United anatoa mchango kwa timu ya Taifa lake ndani na nje ya uwanja kwenye upande wa fedha kipindi chote ambacho Ronaldo anatumikia kikosi cha Ureno timu hiyo imetengeneza faida kila mwishoni mwa mwaka kupitia udhamini kutoka makampuni mbalimbali ambayo yanawekeza timu ya taifa Ureno sababu ya uwepo wa CR7 anayeshikilia rekodi ya ufungaji bora muda wote kwa timu za Taifa Duniani.