Friday , 11th Oct , 2024

Jeshi la Polisi mkoani Singida linawashikilia watuhumiwa wanne ambao ni askari mgambo watatu pamoja na mtendaji wa kijiji kwa tuhuma ya kuhusika na mauaji ya Frank Joseph Mnyalu miaka 28, ambaye imedaiwa kuwa alishambuliwa na watuhumiwa hao mpaka kupelekea kifo chake akiwa anapatiwa

Jeneza la Frank Mnyalu

matibabu huku watuhumiwa hao wakidai kuwa marehemu alifanya fujo ofisini kwao.

Akizungumza Kamanda wa Polisi mkoa wa Singida SACP Amon Kakwale amesema katika kipindi cha mwezi Septemba jeshi hilo limefanikiwa kuwakamata watuhumiwa 49 wa makosa mbalimbali ikiwemo watuhumwa hao wanaodaiwa kumuua Joseph Mnyalu mkazi wa Kata Mhintiri wilayani Ikungi.

"Jeshi la Polisi Mkoa wa Singida linawashikilia watuhumiwa wanne ambao ni Joackim Marko (36) afisa mtendaji wa kijiji cha Mhintiri, Emmanuel Daudi (42), Yona Ramadhan (40) na Dominiko Stephano (38), wote ni askari mgambo na wakaazi wa Mhintiri kuhusiana na mauaji ya Frank Joseph Mnnyalu (28) mkulima na mkazi wa Kijiji na Kata ya Mhintiri, Tarafa ya Ihanja, Wilaya ya Ikungi aliyefariki dunia akiwa anapatwa matibabu katika kituo cha afya Ihanja baada ya kushambuliwa ofisini na watuhumiwa hao kwa tuhuma za kufanya fujo," Amesema kamanda Kakwale

Hata hivyo kamanda Kakwale ameendelea kubainisha kuwa watu wengine waliokamatwa ni watuhumiwa waliokutwa na dawa za kulevya aina ya bangi na mirungi, huku ambapo mmoja ni mtuhumiwa aliyekamatwa kwa kosa la kusafirisha mwanafunzi wa kike kutoka Singida kwenda Arusha kufanya kazi za ndani.