Thursday , 19th Sep , 2024

Serikali kupitia Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, imetangaza kujenga vituo vya zana za kilimo nchi nzima na kuanza kugawa ruzuku ya mbegu za mahindi huku Bashe akiahidi kula sahani moja na wafanyabiashara vishoka wanaonyonya wakulima.

Waziri wa Kilimo Hussein Bashe

Hayo yameelezwa leo katika muendelezo wa ziara ya kikazi ya Waziri Bashe akiwa mkoani Ruvuma katika kituo cha ununuzi wa mahindi Madaba.

"Wapo wafanyabishara wanaonya na kula jasho la wakulima bila uoga bei elekezi ya mahindi ni sh 700 kg lakini wao wananunua kwa sh 300, mpunga kg 1 ni sh 900 kg 100 sh 81,000 wao wananunua kg 1 kwa sh 600 hii hatutajubali," amesema Bashe

"Sina tatizo na wafanyabishara lakini sitavumilia unyonyaji uliopitiliza tutajenga maghala kila sehemu hawataki kununua naiagiza Mamlaka ya Hifadhi ya Chakula (NFRA), kuhakikisha inanunua mazao hayo nchi nzima mpaka kabla ga msimo wa kilimo kuisha," ameongeza.

Amesema Serikali inatambua adha wanayokutana nayo wakulima kutokana na uhaba wa zana za kilimo, na maumivu wanayokutana nayo katika kukodi Trekta, pawatila, ulanguzi katika mbegu, mbolea.

Amesema, serikali katika katika kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa na tija na kufika masoko ya kimataifa na kuifanya sekta hiyo kuinua uchumi imeamua kuwekeza.

Ameeleza katika vituo hivyo kutakuwa na zana za kilimo kama matrekta na zana zake zikiwemo plau, haro, planters, boom sprayers na tela za kusafirishia mizigo pamoja na Combine Harvester

Waziri Bashe ameitaja mikoa itakayonufaika na awamu ya kwanza ya ujenzi huo kuwa ni Mwanza, Simiyu, Geita, Shinyanga, Kigoma, Mara, Tabora, Singida,Katavi, Shinyanga, Mbeya, Njombe, Ruvuma, Tanga, Dodoma.

"Tumetambua kuwa wakulima wanakodishiwa zana hizo kutoka sh. 60,000 hadi 120,000 hii si sawa na  kuumiza wakulima na hawawezi kuona tija katika kilimo serikali imeamua italeta zana hizo ikiwemo matrekta na wakulima watakodi kwa bei elekezi ya sh 35,000 hadi 40,000 haitazidi hapo,"amesema.

Amesema mwakani pia serikali itasambaza mashine za kusafishia mahindi, mtama na mazao mengine lengo ni kuona bidhaa hizo zinakidhi viwango vya soko la kimafaifa na itatenga fedha ya kununu nafasi zisizo an ubora kwa ajili ya chakula cha mifugo ili kuwapungizia hasara wakulima.