Friday , 13th Sep , 2024

Katika kuadhimisha miaka 25 tangu kufariki kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, Klabu ya baiskeli ya Twende Butiama kwa kushirikiana na wadau imetangaza mbio za msafara wa baiskeli za Twende Butiama Mwaka 2024 ambazo zitaanza kufanyika Septemba 28 katika Mikoa 12.

Akizungumza mapema Leo jijini Dar es Salaam Mwanzilishi wa mbio za baiskeli zenye kampeni ya Twende Butiam,Gabriel Landa amesema mbio hizo zinaadhimisha urithi wa Baba wa Taifa kupitia uendeshaji baiskeli, shughuli za kijamii na hisani.
-
"Tunatarajia kugawa madawati kwa Wanafunzi katika Mikoa yote 12 na kupanda miti kulingana na umri ambao mtu yuko nao hii ni kuenzi utendaji kazi wa baba wa Taifa.Tunawakaribisha waendesha baiskeli wa ngazi zote kutoka ndani na nje ya Tanzania kujiunga nasi kwenye tukio hili la siku 14 na kufikia zaidi ya Kilomita 1500 katika mikoa 12 nchini,” amesema Gabriel Landa.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Mahusiano na Vodacom Tanzania Foundation, Zuweina Farah amesema kuwa Juhudi hizi zinaendana na malengo yao ya kuwawezesha watu na kulinda ustawi wa sayari yetu.
-
"Tunawahimiza waendesha baiskeli wote wa umbali mrefu na mfupi kujisajili na kuungana nasi kufanikisha jambo hili. Hii ni pamoja na wadau wengine na wapenda maendeleo walio tayari kushirikiana nasi,” amesema Zuweina Farah.

-
Msafara huu wa Twende Butiama ulianzishw na kikundi cha waendesha baiskeli mwaka 2019 na ili kuadhimisha upendo wa Mwalimu Nyerere wa kuendesha baiskeli na maono yake kimaendeleo katika maeneo matatu muhimu ambayo ni elimu, afya na utunzaji wa mazingira ambayo yanaweza kuwasaidia Watanzania kupiga hatua kijamii na kiuchumi.