Tuesday , 30th Jul , 2024

Meli kubwa iliyobeba mizigo tani elfu 14 imetia nanga katika bandari ya Tanga kutoka nchini China kwa mara ya kwanza baada ya uboreshwaji mkubwa wa bandari hiyo uliogharimu zaidi ya shilingi bilioni 429.

Meli

Meli hiyo imebeba magari zaidi ya 300 ya mizigo ambayo yatasafirishwa kwenda nchi za DRC Congo, Zambia, Burundi na Rwanda ambapo inatarajiwa kukaa bandarini hapo kwa muda wa siku tatu na kuondoka.

Akishuhudia mapokezi ya meli hiyo, Naibu Waziri wa Uchukuzi David Kihenzile amesema fedha zilizowekezwa katika maboresho hayo zimeanza kuonesha mafanikio makubwa kwani utendaji kazi katika bandari hiyo umekuwa na tija kubwa kwa Taifa. 

"Mwaka 2019/2020 idadi ya meli jumla zote zilikuwa 118 mwaka uliofuatia yaani 2020/2021 zilikuwa meli 113 ziliongezeka kidogo kidogo lakini ilipofika 2021/2022 zikawa 198 lakini leo mwaka wa fedha ulioisha tumefikisha meli 307 fikiria kutoka kwenye meli 118 2019/20 leo zimefika meli 307 ni takribani mara mbili au mara tatu hii inadhihirisha fedha iliyowekezwa hapa haikutupwa na watendaji hawakulala usingizi, "amesema Kihenzile. 

Naye Mkuu wa Mkoa wa Tanga Balozi, Dkt. Batilda Burian amesema mkoa upo kimkakati ambao una uwezo kibiashara na maboresho hayo yatapunguza wigo wa wafanyabiashara kurundika mizigo bandari ya Dar es Salaam kwa kuipitishia Tanga.