Saturday , 27th Apr , 2024

Kuelekea maandamano ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yanayotarajiwa kufanyika Aprili 30, 2024 mjini Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro wakazi wa Mkoa huo wametakiwa kutambua kuwa maandamano hayo sio kelele za wahuni bali ni ya amani kwa ustawi wa Tanzania

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa

Akizungumza na vyombo vya habari mjini Moshi leo Aprili 27, 2024 Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini Amani Golugwa amesema Watanzania wanaaminishwa kuwa maandamano hayo ni ya wahuni na wapiga kelele na kwamba huko ni kuwakosea watanzania wanaokabiliwa na hali ngumu za maisha. 

"Kama unanunua sukari kilo shilingi 1000 usiandamane kaa nyumbani, maandamano haya hayatakoma, tutaandamana pia katika ngazi za wilaya mpaka serikali ielewe," amesema Golugwa.

Golugwa amesema  Jeshi la Polisi mkoani Kilimanjaro limetoa ushirikiano mzuri ambapo njia zilizoruhusiwa ni tatu na mkutano wa hadhara utafanyika katika Viwanja vya Mashujaa ambako viongozi wa Chadema watakuwepo.

Mwenyekiti wa Chadema Freeman Mbowe, ataongozana na Boniphace Mwabukusi, Peter Msigwa, Godbless Lema, Raymond Mboya, John Heche na Japhary Michael pamoja na viongozi wengine wa ngazi za Kijiji, Kata na Wilaya.