Friday , 26th Jan , 2024

Diwani wa Kata ya Ilenda, Halmashauri ya Buchosa, Sengerema mkoani Mwanza kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Mneke Mauna anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, akituhumiwa kumshambulia na kumpiga makofi Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo, Lazaro Lubalika.

Diwani wa Kata ya Ilenda (Kulia) ambaye anashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoani Mwanza akituhumiwa kwa kosha la kumshambulia na kumpiga makofi Mwenyekiti wa CCM wa kata hiyo, Lazaro Lubalika (Kushoto)

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrord Mtafungwa amethibitisha kukamatwa kwa diwani huyo kwa kesi ya shambulio la kudhuru mwili na kueleza kuwa uchunguzi unaendelea.

“Ni kweli tunamshikilia kwa kosa la shambulio la kumpiga makofi hadharani mwenyekiti wa CCM, Kata ya Ilenza, Lazaro Lubalika na kumsababishia maumivu. Tunaendelea na mahojiano na itakapothibitika atafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazomkabili,” alisema Mtafungwa.

Inadaiwa kuwa tukio hilo lilitokea Januari 20, 2024 majira ya saa tisa alasiri baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa kuziba nafasi ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Kata ya Ilenza, baada ya aliyekuwepo awali kufariki dunia.

Akizungumzia tukio hilo mbele ya waandishi wa habari, Lubalika alisema baada ya kumalizika kwa uchaguzi huo, alikwenda nyumbani kwake kwa ajili ya kubadilisha nguo na baadaye kurejea eneo maarufu la Senta kwa ajili ya kuendelea na shughuli zake za kumpatia kipato.

Lubalika aliendelea kueleza kuwa baada ya kurejea Senta, alimwona diwani huyo akiwa amekaa na wananchi wengine ambapo alimuita kwa ishara na alipofika, diwani huyo alianza kumtolea maneno makali akimtuhumu kuunda genge la wahuni.  

“Baada ya kunitolea tuhuma hizo, nilimuuliza kama alikuwa na uthibitisho na tuhuma hizo? Nikashangaa akinivamia na kunipiga makofi, kitendo kilichonisababishia maumivu na kunifedhehesha sana,” alisema.

Baada ya tukio hilo, mwenyekiti huyo alienda kuripoti katika Kituo Kidogo cha Polisi cha Nyakaliro na kufungua jalada lenye namba AKO/IRA/24/2024 ambapo mtuhumiwa huyo alianza kusakwa na baadaye kukamatwa na Jeshi la Polisi kwa mahojiano.

Baadhi ya wananchi wa kata hiyo waliozungumza na mwandishi wetu, wamelaani vikali kitendo hicho cha udhalilishaji kilichofanywa na diwani huyo na kuuomba uongozi wa juu wa chama hicho kumchukulia hatua za kinidhamu.

Martin Edward ni miongoni mwa wananchi wa Ilenza walioshuhudia tukio hilo ambaye amesema kitendo hicho siyo cha kiungwana na hatua stahiki zinatakiwa kuchuliliwa dhidi ya diwani huyo.