Akizungumza na Kurasa nyumbani kwa marehemu Komba. Mmoja wa watoto wake Gerard Komba amesema mara baada ya kuagwa kwa mwili huo hapo kesho utasafirishwa hadi katika kijiji cha Lituhi wilayani Mbinga tayari kwa maziko yatakayofanyika kesho kutwa siku ya Jumanne.
Rais Jakaya Kikwete ni miongoni mwa viongozi waliofika nyumbani kwa marehemu Komba leo, kuifariji familia ya marehemu akiambatana na mkewe Mama Salma Kikwete.
Akitokea mjini Dodoma akiwa ameambatana na viongozi mbalilmbali wa chama cha mapinduzi, pamoja na mkewe mama Salma Kikwete, Rais Kikwete ametia saini kitabu cha maombolezo na kisha kuzungumza na familia ya marehemu Kaptein John Komba mbunge wa Mbinga na kuzungumza na viongozi mbalimbali wa chama, serikali ndugu jamaa na marafiki waliofika nyumbani kwa marehemu maeneo ya Mbezi Tangibovu jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na waandishi wa habari spika wa bunge Mhe. Anna Makinda amesema pengo la kiongozi huyo halitaweza kuzibika kutokana na ucheshi uliomfanya kupendwa na wabunge wengi zaidi na kuwataka wabunge kufanya kazi kwa neema ya mungu na watakapoondoka watakuwa wametimiza wajibu wao.
Wakizungumza na waandishi wa habari naibu katibu mkuu wa CCM, Mhe. Mwigulu Mchemba amesema kifo cha marehemu Kaptein John Komba ni pigo kubwa kwa CCM kwa kuwa ni alama ya chama cha mapinduzi na kuwataka wana CCM kuyaenzi matendo ya marehemu Kapten Komba, huku waziri mkuu mstaafu Mhe. Edward Lowasa akiwataka wana CCM na wananchi kwa ujumla kumuenzi marehemu kwa kuiangalia familia yake.
Akielezea taratibu za maazishi, mtoto wa marehemu Gerald Komba ametoa shukrani kwa vyama vya siasa, viongozi wa serikali, jamaa na marafiki walioikimbilia familia hiyo katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na baba yao ambapo amesema mwili wa marehemu unatarajiwa kuzikwa siku ya Jumanne kijijini kwake Manda au Litui mkoni Ruvuma siku ya Jumanne Machi 3 mwaka huu.