Waziri Mkuu Mizengo Pinda akiwa ziarani wilayani Ngorongoro alipokwenda kufanya mkutano na watu wa jamii za wamasai na wasonjo Septemba, 2013
Wananchi na viongozi wa jamii za Wamasai na Wasonjo wilayani Ngorongoro mkoani Arusha wamesema wako tayari kuwafichua watu wanaoingiza na kuuza silaha za kivita na risasi zake katika maeneo yao ambazo zimekuwa zikitumika kuua watu wasio na hatia.
Wananchi hao wameyasema hayo katika kikao maalumu cha usuluhishi wa mgogoro wa muda mrefu miongoni mwa jamii hizo kilichoshirikisha viongozi wa ngazi mbalimbali wakiwemo wa serikali, dini na viongozi wa mila ambao madiwani wa kata za Samunge na Olorieni wamelishwa kiapo cha kimila cha kusimamia amani katika eneo hilo.
Akizungumza katika kikao hicho katibu mwenezi wa CCM mkoa wa Arusha aliyekuwa mgeni rasmi Joseph Issack amewataka viongozi wote wa chama na serikali kuacha kuwafumbia macho watu wanaochezea amani na diwani atakayebainika kuchochea mauaji atavuliwa madaraka
Baadhi ya wazee wa mila wa jamii hizo wameendelea kuitaka serikali kuwa macho kwani wapo baadhi ya watu wanaotaka kutumia tofauti za jamii hizo kutaka kuvunja amani kwani licha ya kuwa tofauti zao zilianza zamani tangu enzi za aliyekuwa waziri mkuu hayati Edward Sokoine walikuwa wanazimaliza kwa mazungumzo na wala sio kwa kutumia silaha za kivita .
Mgogoro huo wa ardhi unadaiwa kuwa umeanza mwaka 1975 na umekuwa ukiibuka mara kwa mara na kupoa hasa wakati msimu wa kilimo na kusuluhishwa kwa njia za mazungumzo bila mapigano wala umwagaji wa damu lakini miaka ya hivi karibuni umekuwa ukisababisha mapigano tena ya kutumia silaha za kivita na umesababisha vifo na uharibifu mkubwa mali.