Monday , 6th Nov , 2023

Kutokana na mkoa wa Geita kushika nafasi ya tano kwa matukio ya mauaji na vitendo vya ukatili hapa nchini jeshi la polisi mkoani Geita limezindua kampeni ya Ongea nao yenye lengo la kutoa elimu kwa jamii ili kutokomeza vitendo vya mauaji na ukatili vinavyofanyika katika jamii

Kampeni ya Ongea Nao imezinduliwa na mkuu wa mkoa wa Geita Martine Shigela katika ukumbi wa EPZA uliopo mjini Geita ambapo Mkuu wa Jeshi la polisi mkoani Geita ACP Safia Jongo amesema chanzo kikubwa cha ukatili na mauaji katika mkoa wa Geita ni imani za kishirikina maeneo ya migodini

"Chanzo kikubwa ukiwakamata watuhumiwa wanakili kwamba ni imani za kishirikina kwamba mganga amemwambia akibaka mtoto wa miaka mitatu basi shimo lake litatoa dhahabu nyingi ndo maana kwenye hutuba yangu nimeeleza kwamba nitaenda hata kwenye machimbo madogomadogo ili kutoa elimu wachimbaji waweze kuchimba kisasa ili kuondokana na imani za kishirikina ili kulimaliza swala hili la ukatili katika jamii ndo maana kama jeshi la polisi tumezindua kampeini hii ya ongea nao ili tuweze kuongea na jamii ili kushusha matukio ya kiarifu chanzo chake ambacho ni ukatili wa aina mbalimbali” - ACP Safia Jongo  RPC Mkoa wa Geita

Aidha Kamanda Jongo amesema matukio ya mauaji kwa mkoa wa Geita yamepungua kutoka matukio 49 mwaka jana hadi matukio 32 mwaka huu.

“Kwa mfano mwaka jana tulikuwa na matukio ya mauaji 49 january tu Octoba lakin mwaka hii tuna matukio 32 kwaiyo unaweza kuona ni matukio chanya kwetu lakini matukio ya ubakaji mwaka jana yalikuwa 86 na mwaka huu ni matukio 75 matukio ya kulawiti mwaka jana yalikuwa 7 na mwaka huu ni matukio 6 lakini matukio ya shambulio la kudhuru mwili mwaka jana yalikuwa matukio 26 na mwaka huu ni matukio 21 na matukio ya mimba shuleni mwaka jana yalikuwa 27 na mwaka huu 25” ACP Safia Jongo  RPC Mkoa wa Geita.

“Nawaagiza kila mmoja atomize wajibu wake ukiwa kama mwenye kiti wa kitongoji,wa mtaa ,wa kijiji au mtendaji hata balozi wa Nyumba kumi wa chama chetu chama cha mapinduzi anaowajibu wa kuhakikisha ukatili wa kijinsia na watoto anaudhibiti katika eneo lake la utawala” - Martine Shigela, Mkuu wa mkoa wa Geita.

Kwa upande wao wadau wanaopambana na vitendo vya ukatili katika jamii wamesema wapo tayari kutoa ushirikiano kwa jeshi la polisi mkoani Geita ili kutokomeza kabisa vitendo vya ukatili katika Jamii.

“Sote tukiungana kwa pamoja sisi wanaopambana na ukatili kwenye jamii pamoja na wale wanaofanya vitendo vya ukatili wakipewa elimu tunaweza kuvitokomeza kabisa vitendo hivi katika jamii yetu” - Anuary Aziz, Mwanaharakati wa kupambana na ukatili wa kijinsia

“Sisi tutatumia sanaa yetu kuakikisha tunavipinga na vikomesha vitendo vyote vya ukatili wa kinjia katika jamii yetu”KELVIN MASATU Msanii wa Bongo Movie