Thursday , 7th Sep , 2023

Wakazi wa Kijiji cha Mwabomba Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga ambao ni wachimbaji wadogo wa madini, wamesema ujenzi wa Barabara umetatua changamoto ya kutumia gharama kubwa kusafiri pamoja na kulazimika kupanda mitumbwa ili kuvushwa kutokana na Barabara kujaa maji.

Shughuli kubwa za kiuchumi zinazofanyika katika Kijiji cha Mwabomba Halmashauri ya Ushetu Wilayani Kahama ni uchimbaji wa madini ambapo wanahitaji kuwa na miundombinu bora ya Barabara kwa ajili ya kusafirisha mizigo yao kama wanavyobainisha.

Manugwa Mihayo mkazi wa Kijiji cha Mwabomba amesema kwa sasa wanaishukuru serikali kwa kuboresha miundombinu baada ya Tanroads kujenga Barabara kwa kiwango cha moramu hatua ambao imewaondolea adha ya Usafiri.

Tulikuwa tunateseka sana hasa wakati wa masika mtu akihitaji kwenda masumbwe wakati wa masika analazimika kuvushwa kwa mtumbwi lakini baada ya kujengewa Barabara hii tunaende tu kwa magari hali imekuwa nzuri

Mkazi mwingine wa Kijiji hicho Japheth Daudi amesema ujenzi wa Barabara katika eneo hilo ambalo linamsongamano wa watu wengi kutokana na shughuli za kuichumi zinazofanyika umekuwa na tija kubwa kutokana na kuwaondolea usumbufu waliokuwa wakipata awali. 

Samwel Mhoja mkazi wa Mwabomba ameiomba Tanroads kutoa elimu kwa jamii ili waache kuharibu miundombinu ya Barabara pamoja na kuyadhibiti magari makubwa ambayo yanapita katika eneo hilo yakiwa na uzito mkubwa ambao ni chanzo cha uharibifu wa Barabara.

Akizungumzia ujenzi wa Barabara Meneja wa Tanroads Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi amesema bado kuna changamoto ya uharibifu wa miundombinu hiyo pamoja na kuweka matuta Barabara kiholela.

Tanroads Mkoa wa Shinyanga inasimamia Barabara zenye urefu wa kilomita 1178 huku lengo ni kuhakikisha zinapitika wakati wote.