Monday , 19th Jun , 2023

Watu wasiopungua 13 wamepoteza maisha na maelfu ya watu kuyakimbia makaazi yao baada ya kimbunga kukumba eneo la kusini mwa Brazil.

 

Mvua kubwa na upepo mkali siku ya Alhamisi na Ijumaa vilisababisha uharibifu katika miji kadhaa katika jimbo la Rio Grande do Sul, ikiwa ni pamoja na mji mkuu wake Porto Alegre, ambao ni wa hivi karibuni katika msururu wa majanga yanayohusiana na hali ya hewa kuikumba nchi hiyo kubwa ya Amerika Kusini.

Mtoto wa miezi minne ni miongoni mwa waliofariki, kwa mujibu wa vyombo vya habari vya eneo hilo, ambavyo vilitangaza picha za gari lililokuwa limesombwa na upepo mkali.

Karibu watu 5,000 waliachwa na nyumba zilizoharibiwa na siku ya Jumapili watu 84,000 hawakuwa na umeme.

 Siku ya Jumapili, mitaa katika miji ya Novo Hamburgo, Lindolfo Collor na Sao Leopoldo bado ilikua imefurika. Wakati mvua ikiendelea, wanajeshi waliweza kufanya shughuli za uokoaji katika mji wa Novo Hamburgo.

Brazil imekumbwa na mfululizo wa majanga ya hali ya hewa katika miaka ya hivi karibuni, ambayo wataalamu wanasema yanafanywa kuwa mabaya zaidi na mabadiliko ya hali ya hewa.