Monday , 12th Jun , 2023

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaelekeza wakuu wa mikoa wakae na mabaraza ya biashara na wamiliki wa kumbi za starehe katika mikoa yao kwa madhumuni ya kutafuta muafaka wa pamoja katika utekelezaji wa sheria, kanuni, mwongozo kuhusu udhibiti wa athari zitokanazo na sauti zilizozidi viwango

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa

Waziri Mkuu amezielekeza idara za mipangomiji katika halmashauri za wilaya zote nchini zitenge maeneo ya ujenzi wa nyumba za ibada kama wanavyotenga maeneo ya taasisi nyingine. 
 
Ametoa maelekezo hayo leo Juni 12, 2023, jijini Dar es Salaam, wakati akizindua kongamano la kujengewa uelewa kuhusu madhara yatokanayo na sauti zilizozidi viwango katika nyumba za ibada, lililoandaliwa na Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT).

"Kwa upande wa udhibiti wa sauti zilizozidi, kila mamlaka iliyotoa vibali au leseni ya shughuli au biashara, zifuatilie mwenendo wa matumizi ya leseni hizo, nasisitiza kuwa kila mamlaka itimize wajibu wake kulingana na maelekezo yaliyimo katika Mwongozo wa Uthibiti wa Uchafuzi wa Mazingira Utokanao na Kelele na Mitetemo uliotolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais," amesema Waziri Mkuu
 
Akizungumzia kuhusu wamiliki wa majengo, Waziri Mkuu amewataka wafanye tathmini ya athari ya mazingira kwa watu wanaotumia majengo hayo pamoja na wakazi wa jirani na majengo hayo kwa lengo la kubaini madhara kwa watumiaji wa majengo hayo na jamii inayozunguka. 
 
Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasisitiza viongozi wa dini, wanaoshiriki katika kongamano hilo waendelee kuwa vielelezo na mabalozi wazuri wa kufikisha yale mambo mazuri yanayowasilishwa katika kongamano hilo. 
 
Naye, Mkurugenzi Mkuu wa NEMC, Dkt. Samuel Gwamaka amesema madhumuni ya kongamano hilo ni kuwakutanisha pamoja viongozi wa dini na mila ili kutoa elimu ya athari za sauti zilizozidi viwango kutoka kwenye nyumba za ibada na jamii.

Amesema kanuni za udhibiti wa kelele na mitetemo za mwaka 2015 zimeainisha viwango vinavyoruhusiwa katika maeneo ya makazi, nyumba za ibada, biashara, viwanda na hospitali kwa ajili ya jamii, mfano viwango vya sauti vinavyoruhusiwa katika nyumba za ibada zilizopo maeneo ya makazi ni dBA 60 wakati wa mchana na usiku dBA 40.

Amesema sauti zinazozidi viwango katika nyumba za ibada zinaweza kuathiri afya za waumini waliopo  kwenye nyumba za ibada na maeneo ya jirani na kusababisha matatizo ya kusikia, usingizi na kuathiri uwezo wa kufanya kazi pamoja na kusababisha migogoro kati ya wakazi na viongozi au waumini.