Sunday , 10th Jul , 2022

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb), amewataka watumishi wa Wizara ya Ulinzi na JKT kuendeleza utii, weledi na uaminifu katika utekelezaji wa majukumu yao ya kazi, na kuepuka migogoro mahali pa kazi.

Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Stergomena Lawrence Tax (Mb) akiwa kwenye kikao na watumishi wa wizara hiyo

“ Pamoja na kuwa sina mashaka kuhusu nidhamu mliyonayo katika kazi, naendelea kusisitiza kuendeleza utii, weledi na uaminifu katika utekelezaji wa majukumu yenu ya kazi, na kuepuka migogoro mahali pa kazi”, alisema Dkt. Stergomena.

Dkt. Stergomena ameyasema hayo wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi na vyeti kwa wafanyakazi bora kwa mwaka 2022, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Ofisi ndogo ya Wizara - Upanga, Jijini Dar es Salaam. Mheshimiwa Waziri pia, amewashukuru watumishi wote kwa utendaji wao, pamoja na changamoto kadhaa wanazokabiliana nazo, wameendelea kujitoa na kutumia weledi wao katika kutekeleza majukumu mbalimbali.

“Nitumie fursa hii pia, kuwashukuru watumishi wote kwa utendaji wenu, pamoja na changamoto kadhaa tunazokabiliana nazo, mmeendelea kujitoa na kutumia weledi wenu katika kutekeleza majukumu mbalimbali. Hili ni jambo la kujivunia na ninawapongeza na niwatake kuendelea na moyo huo ili kulijenga Taifa letu”, alisema.

Dkt. Stergomena alibainisha kuwa siku hii ya leo ni muhimu sana, maana wamekusanyika kwa lengo la kukabidhi zawadi kwa wafanyakazi bora, kwa maana hiyo akawasihi na watumishi ambao hawakubahatika kuchaguliwa kuendelea kufanya kazi kwa bidii.

“Sote tumefanya kazi na kuchangia katika mafanikio ya Wizara, hata hivyo, katika ushindani wapo watakaoibuka kidedea. Tunawapongeza washindi, na Wizara inautambua mchango wa kila mmoja. Hivyo tuendelee kujituma na kuwa washindi wa kesho”, alisistiza.