Tuesday , 19th Apr , 2022

Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2020/2021 imebainisha kuwa SELF Microfinance imetenga asilimia 56 ya fedha zake zote kwa shughuli zisizo za msingi na vikundi vya kijamii visivyolengwa.

Mfano wa Noti za Tanzania

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, mapitio ya taarifa za fedha zilizokaguliwa yalionyesha kuwa, SELF Microfinance iliwekeza kwa kiasi kikubwa kwenye dhamana za soko kupitia FDR, bondi na T-Bills ambazo haziwiani na shughuli zake kuu za biashara ambazo ni utoaji wa mikopo kuanzia 2016/2017 hadi 2019/2020.

Katika kipindi cha 2017/2018 hadi 2020/2021, SELF Microfinance iliwekeza asilimia 56 ya fedha zake kwenye benki za biashara kinyume na matakwa ya Sera ya Mikopo ya 2019.

Mradi wa SELF ulikuwa miongoni mwa programu za Serikali zinazotekeleza jukumu la kupunguza umaskini kwa niaba ya Serikali ambayo ilifadhiliwa kwa pamoja na Serikali ya Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika.

Mradi ulilenga katika kuongeza mchango wa Wafanyabiashara Ndogo Ndogo (SMEs) katika kukuza uchumi na kupunguza umaskini na kuimarisha sekta ya mikopo midogo midogo nchini Tanzania.