Tuesday , 19th Apr , 2022

Soko la hisa la Dar es salaam limerekodi mauzo ya bilioni 10.6 katika kipindi cha wiki mbili za mwanzo za mwezi Aprili, kiasi ambacho ni sawa na karibu theluthi moja ya mauzo ya robo mwaka katika robo ya kwanza ya mwaka huu ambapo wawekezaji wa kigeni wamehusika zaidi kununua na kuuza hisa

Soko la Hisa la Dar es Salaam

Ripoti ya soko imeonyesha kuwa, wawekezaji wa kigeni walisalia kuwa wahusika wakuu katika kipindi kilichohakikiwa katika shughuli za uuzaji na ununuzi ambapo waliingiza bilioni 9.02 kupitia ununuzi wa hisa, ambayo ni sawa na asilimia 85.02 ya thamani yote ya ununuzi, wakati wawekezaji wa ndani wanaonunua hisa walikuwa asilimia 14.98.

Aidha, kwa mujibu wa ripoti hiyo, wawekezaji wa kigeni pia walitawala shughuli ya kuuza, baada ya kurekodi mauzo ya bilioni 8.39 ambayo ni sawa na asilimia 79.08 ya mauzo yote, huku wawekezaji wa ndani wakiingiza asilimia 20.92 ya thamani hiyo.

Ripoti hiyo inaonyesha, wakati wa kufunga kikao cha wiki iliyopita, soko lilipewa hisa nyingi zaidi kuliko zabuni, huku kaunta za kampuni za uwekezaji za Vodacom, NICO, CRDB na TCCIA zikiwa na zaidi ya hisa 100,000 kwa kila moja.