Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Khalist Luanda
Serikali imetangaza matokeo ya awali ya uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Jumapili iliyopita ambapo hadi sasa matokeo yaliyokusanywa ni kutoka katika vijiji 9,047 na mitaa 3,078.
Matokeo hayo yanaonesha kuwa Chama Cha Mapinduzi CCM kimeongoza uchaguzi huo kwa kujinyakulia vijiji 7,290 sawa na 80.58% na mitaa 2,116 sawa na asilimia 68.7% huku chama kikuu cha upinzani CHADEMA kikijinyakulia vijiji 1,248 sawa na 13.8% na mitaa 753 sawa na 24.5%, Chama cha wananchi (CUF) ikishinda katika vijiji (946).
Akitangaza matokeo hayo Mkurugenzi wa Uchaguzi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Khalist Luanda amesema kuwa mbali na vyama hivyo vikubwa viwili kushika nafasi ya juu, chama cha wananchi CUF kimeibuka nafasi ya Tatu kwa kujinyakulia vijiji 382 na mitaa 235 kikifuatiwa na NCCR Mageuzi, TLP, NLD, ACT na UNDP
Taarifa hiyo pia ikazungumzia sehemu ambazo bado hazijafanya uchaguzi huo ambapo baadhi ya maeneo katika wilaya 18 na wilaya 3 zinatarajiwa kufanya uchaguzi huo Jumamosi ijayo huku pia ikikataza kampeni za aina yeyote na chama kitakachopuuza agizo hilo kitakuwa kimekiuka taratibu za uchaguzi na mgombea wake anaweza kuondolewa
Taarifa hiyo pia ikaanisha mikoa ambayo imefanya uchaguzi bila kuwepo kwa kasoro yoyote ni pamoja na Arusha, Lindi, Mtwara, Ruvuma, Dodoma, Katavi, Kagera na mingine ni Mbeya, Singida na Njombe