Thursday , 4th Dec , 2014

Jeshi la polisi mkoa wa Mara limetangaza kuchukua hatua kali dhidi ya waendesha pikipiki maarufu kama bodaboda ambao wamekuwa wakijichukulia sheria mkononi pindi ajali zinapotekea.

Mmoja wa Waendesha Pikipiki Maarufu kama Boda boda akiongozana na Askari wa Usalama Barabarani.

Kamanda wa polisi mkoa wa Mara kamishina msaidizi wa Polisi ACP Philip Kalangi, akizungumza wakati wa ufunguzi wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoani humo, amesema kuwa jeshi la polisi kuanzia sasa halitavumilia ukiukwaji huo mkubwa wa sheria za nchi, huku mkuu wa kikosi usalama cha usalama barabarani mkoa wa Mara mrakibu wa polisi Robert Hussein akitangaza mikakati mbalimbali ya kukabiliana na wimbi la ajali za barabarani.

Akisoma hotuba ya mkuu wa mkoa wa Mara Kapt Mstaafu Aseri Msangi, katibu tawala wa mkoa wa Mara Bw Benedict ole Kuyani, amewataka askari wa kikosi cha usalama barabarani kuchukua hatua kali katika usimamizi wa sheria hizo ambazo zimekuwa zikikiukwa na madereva hao kwa uzembe.

Katika ufunguzi huo wa wiki ya nenda kwa usalama barabarani mkoani Mara ambayo yamepambwa na maandamano ya vyombo mbalimbali vya moto wakiongozwa na askari wa usalama barabarani, imeelezwa kuwa katika kipindi cha Januari hadi Oktoba mwaka huu jumla ya ajali 58 zimetokea kwa mkoa wa kipolisi wa Mara na kusababisha vifo vya watu 65 huku 238 wakijeruhiwa.