Sunday , 25th Oct , 2020

Virusi vya Covid-19 maarufu kama Corona, vilitangazwa kwa mara ya kwanza kuwa vimeingia nchini Tanzania, Machi 16, 2020. Tangu wakati huo, hofu iliwakumba watanzania na hatimaye, ikatolewa amri ya ofisi, shule na baadhi ya shughuli za kibiashara kufungwa. 

Mfano wa Madarasa yalivyokuwa wazi kipindi cha mlipuko wa COVID-19, Tanzania.

VITA DHIDI YA COVID-19, KUFUNGA SHULE NA VYUO
 
Hofu kubwa zaidi pengine ilikuwa kwa maambukizi hayo kuwapata wanafunzi, ambao huenda wakashindwa kujilinda kwa ufasaha dhidi ya maambukizi hayo. Hivyo basi miongoni mwa hatua za awali kabisa za kujikinga na maambukizi hayo ilikuwa ni kufungwa kwa shule zote za awali, za msingi hadi sekondari hadi hapo serikali itakapotangaza tena kufunguliwa kwa shule hizo. .  

Tangazo hilo lilitolewa jijini Dar es salaam na Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa akisema, “Mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo ya lazima imesitishwa kuanzia sasa ikiwemo shughuli za michezo, semina, matamasha ya muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali za shule na shughuli nyingine za kijamii ambazo si muhimu. Lakini pia tumefunga shule zote za awali, msingi na sekondari hadi kidato cha sita na zitafungwa kwa siku 30 kuanzia leo Machi 17, 2020.”

Na kuongeza kuwa,” Wizara itafanya marekebisho ya ratiba ya kidato cha sita ambao wanatarajiwa kufanya mitihani tarehe 4 mwezi wa Mei. Watakuwa na muda mfupi kwa hiyo itasogezwa tena mbele kadiri ya matokeo yatakavyojitokeza ili nao wapate nafasi ya kusoma kwa kipindi kile kile kilichokubalika kwa mujibu wa ratiba hiyo.

Hata hivyo, licha ya changamoto hiyo, wadau wa elimu waliangalia namna ya kuendelea na masomo wakati wanafunzi wakiwa nyumbani. Na miongoni mwa njia hizo ilikuwa si nyingine bali Teknolojia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA)
 
KUSOMA KWA NJIA YA MTANDAO (TEKNOHAMA)

Baada ya shule kufungwa walimu na wadau wa elimu walitumia vyombo vya habari, zikiwamo Televisheni na  redio kutoa elimu wakati wanafunzi wakiwa nyumbani.

Mbali na mbinu hizo kuna baadhi ya shule zilitumia teknolojia yaani makundi ya whatsap, email na elimu kwa njia ya teknolojia ya Zoom,  kuendelea na masomo kwa wanafunzi wa madarasa yenye mitihani ikiwemo darasa la nne, darasa la saba, kidato cha Pili na cha Nne pamoja na kidato cha Sita. Ambapo wanafunzi, walimu na wazazi walikuwa na maoni tofauti kuhusu teknlojia na changamoto zake.

WANAFUNZI WANAIZUNGUMZIAJE TEKNOHAMA?

Elia Kimaro ni mwanafunzi wa kidato cha Nne katika shule moja ya Sekondari binafsi jijini Dar es Salaam, pamoja na Ester Peter wanaelezea namna ambavyo teknolojia imesaidia kuokoa masomo yao kwakuwa kukaa nyumbani bila kujishughulisha na kazi za shule ingewadhoofisha kitaaluma.

“Bila uwepo wa teknolojia tungesahau vitu vingi na tuko kwenye kundi gumu la kuelekea kuhitimu elimu ya kidato cha Nne, tunashukuru ujio wa teknolojia katika kipindi hiki”, anasema Ester

Jasmin Abdallah mwanafunzi wa darasa la Nne anaeleza kuwa kukosekana kwa simu janja (smartphone) katika familia kulimuathiri kwakuwa alikosa masomo kutokana kushindwa kuchangamana na wenzake baada ya kila familia kuzuia wageni majumbani, kwahiyo ilibidi afunge safari kutafuta walimu majumbani na kupatiwa ‘notice’.

"Kilikuwa kipindi kigumu kwetu hakuna simu naishi na bibi, nilikuwa naenda kwa majirani muda mwingin", anasimulia Jasmin

WALIMU WANASEMAJE?

Odilia Blanka ni mwalimu wa shule ya msingi Ukonga anaeleza namna ambavyo virusi vya Corona vilivyowafundisha utamaduni mpya ambao hawakuwahi kuufikiria katika siku za hivi karibuni.

"Mimi binafsi sikuwahi kuitumia simu yangu kufundishia ila kwa kipindi hiki teknolojia imetuokoa walimu, sisi wa shule binafsi tulikosa mishahara kwa kipindi chote tulichokuwa nyumbani kwa baadhi ya shule, lakini tulipambana na kufanikiwa kufunidisha kwa mtandao na wazazi waelewa walikuwa wakitulipa", amesema Mwalimu Odilia.

WAZAZI WANA MAONI GANI KUHUSU MATUMIZI YA TEKNOLOJIA KIPINDI CHA COVID-19

Kanky Mwaigombe ni Mama wa Watoto wa tatu anaeleza namna ambavyo alikuwa na jukumu la kuchapisha kila siku kazi za watoto wake kwakuwa asingeweza kuwaachia watumie simu kwakuwa kila mmoja alitaka aitumie mwenyewe kwanza, hali iliyopelekea gharama za uchapishaji pamoja na intaneti.
 
WIZARA YA ELIMU INASEMAJE?

Katika kipindi cha mlipuko wa Virusi vya Corona,  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, ilizindua urushaji wa vipindi vya masomo kupitia televisheni na Radio. Ambapo uzinduzi huo ulifanywa na Katibu Mkuu wa  Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Leonard Akwilapo.

Akizungumza  na mtandao huu Dkt. Akwilapo anasema kuwa, "Wizara tulitumia teknolojia kuandaa masomo mbalimbali kwa ngazi ya elimu ya awali,elimu ya msingi na elimu ya kutoka Kidato cha  cha kwanza mpaka cha sita,vipindi hivyo vilisambazwa katika vyombo mbalimbali vya habari na tulifanikiwa na  masomo yaliweza kufikia wanafunzi wetu nchi nzima. Lengo kubwa la kutoa vipindi hivi lilikuwa ni kuwaezesha wanafunzi waendelee kujifunza wakati ambapo wako nyumbani baada ya shule kuwa zimefungwa." Dkt.Akwilapo amesema wizara yake iliandaa vipindi hivyo kupitia Taasisi ya Elimu Tanzania. 

Akilizungumzia Baraza la Mitihani Tanzania (NACTE), Dkt. Akwilapo anasema kuwa "Baraza la mitihani la Tanzania liliandaa vipindi  kwa ajili ya maandalizi ya watahiniwa wa kidato cha sita nayo pia yalirushwa kwenye vyombo vya habari na vipindi hivyo viliwawezesha watahiniwa hawa kufanya marudio ya mada mbalimbali na tumekuwa mashuhuda matokeo ya kidato cha Sita ufaulu umeongezeka".