
Wachezaji wa Juve wakishangilia ubingwa wa Serie kwenye vyumba vya kubadilishia nguo uwanja wa Allianz Stadium
Juventus imetwaa taji la 9 mfululizo la Serie A baada ya ushindi dhidi ya Sampdoria, mjini Turin, na kuweka rekodi ya kuwa timu ya kwanza kufikisha idadi hiyo katika ligi tano bora barani Ulaya.
Cristiano Ronaldo aliiongoza Juve kwa bao la ufunguzi baada ya kuunganisha mpira mfupi wa adhabu wa Miralem Pjanic kunako dakika ya 45, kabla ya Federico Bernardeschi kuunganisha mpira wa shuti la Ronaldo uliotemwa na mlinda wa Sampdolia Emil Audero kuweka bao la pili.
Kwa ujumla taji hilo linakuwa la 36 na inaendeleza rekodi ya kuchukua taji hilo tangu msimu wa 2011/2012.Lakini pia kwenye ligi tano bora ni rekodi nyingine wakifuatiwa na Real Madrid wenye mataji 34 ya La Liga.
VITA YA KIATU CHA DHAHABU
Ronaldo alikosa nafasi ya kumkaribia Ciro Immobile wa Lazio mwenye mabaio 34 huku Mreno huyo akiwa na mabao 31, baada ya kukosa penati dakika za lala salama.
Immobile alifunga Hat-trick wakati Lazio ikiiadhibu Verona 5-1 Jumapili iliyopita.
SARRI AWEKA REKODI YAKE
Kocha wa Juventus Mourizio Sarri mwenye umri wa miaka 61 anakuwa kocha wa kwanza kutwaa kikombe kwenye ligi ya Serie A akiwa na umri mkubwa.
REKODI YA DUNIA YA MATAJI MENGI MFULULIZO
Rekodi ya Dunia kwa timu iliyochukua mataji mengi mfululizo, ni Tafea, ambayo ilishinda misimu 15 mfululizo kwenye ligi ya Vanuatu (1994 to 2009), huko kusini ya Pasific.