Sunday , 19th Jul , 2020

Kocha wa Arsenal Mikel Arteta amesema ana matumaini makubwa kuwa mshambuliaji Pierre-Emerick Aubameyang  atasalia katika klabu hiyo.

Pierre-Emerick Aubameyang

Arteta ametoa kauli hivyo baada ya ushindi dhidi ya Manchester City kwenye nusu fainali ya Kombe la FA ambapo Arsenal walishinda 2-0 na kutinga fainali huku mfungaji wa magoli yote akiwa ni Pierre-Emerick Aubameyang.

''Nina uhakika anakwenda kusaini mkataba mpya wa kubaki Arsenal, kila binadamu hupitia nyakati mbaya na nyakati nzuri, lakini baada ya ushindi nina uhakika amefurahia na sasa anaona yupo sehemu sahihi ambayo angetamani kubaki zaidi'', alisema Arteta.

Arteta amesisitiza kuwa baada ya lawama nyingi kwenda kwa Pierre-Emerick Aubameyang  wakati mambo hayakuwa vizuri ndani ya klabu, anadhani sasa ameonesha uwezo wake kwa vitendo na tofauti na angejibu kwa maneno.

Mkataba wa Pierre-Emerick Aubameyang ndani ya Arsenal unamalizika mwezi Juni mwaka 2021 lakini pande mbili hizo zipo kwenye mazungumzo ya kuongeza mkataba lakini imekuwa ikiendeleza kuwa raia huyo wa Gabon ana mpango wa kuondoka.

Baada ya kutinga fainali ya FA, Arsenal sasa inasubiri mshindi kati ya Chelsea na Man United leo kwenye nusu fainali ya pili. Fainali itapigwa Agosti 1, 2020 kwenye uwanja wa Wembley.