Thursday , 11th Jun , 2020

Kiwango cha umaskini kimeelezwa kupungua katika maeneo yote (Mijini na Vijijini), ambapo Waziri wa Fedha na Mipango Dkt Philip Mpango amesema, umaskini umepungua Mijini kutoka 21.7% hadi 15.8% na  maeneo ya vijijini umepungua kutoka 33.3% hadi 31.3%".

Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango

Hayo ameyasema leo Juni 11, 2020 na Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Philip Mpango, wakati akisoma bajeti kuu ya serikali kwa mwaka wa fedha 2021/20 bungeni Dodoma.

Aidha Mpango amesema, "Hadi Aprili 2020 Jumla ya viwanda vipya 8,477 vimeanzishwa nchini, ongezeko hili la viwanda limeongeza utoshelevu wa bidhaa nchini, mathalani uwezo wa uzalishaji wa Saruji umeongezeka kutoka Tani Mil 4.7 2015 hadi Tani Mil 9. 1 mwaka 2019".

Mbali na hilo Waziri Mpango ameeleza kuwa, "Hadi Aprili 2020, Serikali imeboresha miundombinu ya huduma za afya kwa kujenga Zahanati 1,198, Vituo vya Afya 487, Hospitali za Halmashauri 71, za Rufaa 10, za Kanda 3, kuongezeka kwa Bajeti ya vifaa na dawa  kutoka Bil 31, 2015 hadi Bil 269 2019".

Pia amesema, "Hadi Aprili 2020 akiba ya fedha za kigeni ilifikia Dolla za Marekani Bil 5.3, kiasi hiki kinatosheleza mahitaji ya fedha za kigeni ya kuagiza bidhaa nje ya nchi kwa kipindi cha miezi 6 ukilinganisha na Dolla Bil 4.4 cha mwaka 2015".

Aidha makadirio ya matumizi kwa mwaka wa fedha 2019/2020 yalikuwa Tril 33.11, ambapo Tril 20.86, ni matumizi ya kawaida na Tril 12.25 ni matumizi ya maendeleo.

Kwa upande wa ukuaji wa pato la taifa Waziri Mpango amesema, "Ukuaji wa Pato la Taifa unatarajiwa kupungua kutoka maoteo ya awali ya 6.9% na kufikia 5.5% mwaka 2020 ikilinganishwa na 7% mwaka 2019. Hii ni kutokana na mvua nyingi ambazo zimeharibu miundombinu ya usafirishaji nchini na athari za ugonjwa wa COVID–19".

Kwa mwaka 2020/21, Serikali inapanga kutumia jumla ya shilingi trilioni 34.88 kwa matumizi ya kawaida na maendeleo. Kati ya fedha hizo, shilingi trilioni 22.10 zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya bajeti na shilingi trilioni 12.78 kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Fedha zilizotengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida zinajumuisha shilingi trilioni 10.48 kwa ajili ya ulipaji wa deni la Serikali, shilingi trilioni 7.76 kwa ajili ya mishahara na shilingi trilioni 3.74 kwa ajili ya Matumizi Mengineyo (OC) ambayo yanajumuisha shilingi bilioni 481.9 kwa ajili ya matumizi yatokanayo na vyanzo vya ndani vya Halmashauri.

Tazama Video hapo chini