Friday , 17th Apr , 2020

Katika hali isiyo ya kawaida mkazi mmoja wa mkoani Njombe aliyetambulika kwa jina la Kaido Mfilinga (30) aliedaiwa kuwa ni mganga wa kienyeji, amekutwa akiwa amejinyonga na kuacha ujumbe wa maandishi wa kuomba msamaha kwa mizimu.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe, Hamis Issah

Inaelezwa kuwa mganga huyo amejinyonga baada ya kukiuka masharti ya mganga aliedaiwa kumpa kibuyu ambacho kinatajwa kuwa ndicho kimepelekea kifo chake.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Njombe, Hamis Issah amesema baada ya polisi kuwasili eneo la tukio wameukuta mwili wa marehemu pamoja na ujumbe wa maandishi auliouacha kabla ya kuchukua hatua hiyo.

Sambamba na tukio hilo jeshi la polisi mkoa wa njombe linazishikilia mali mbalimbali zinazodaiwa kuwa ni za wizi zikiwemo televisheni, vifaa vya dukani, madawa ya asili ambayo yanadaiwa kutumika katika matukio ya wizi pamoja na vyombo vya muziki vinavyodaiwa kuibiwa kanisani.

Baadhi ya wakazi wa Njombe wamezungumzia jinsi matukio ya wizi mkoani Njombe yanavyofanyika huku wakilipongeza Jeshi la polisi kwa jitihada wanazoendelea kuchukua kuokoa mali hizo.