Thursday , 18th Sep , 2014

Vurugu zimezuka jana asubuhi katika makao makuu ya jeshi la Polisi jijini Dar es Salaam nchini Tanzania, muda mfupi baada ya Mwenyekiti taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo – Chadema, Freeman Mbowe, kuwasili kwa ajili ya mahojiano.

Mbowe aliitwa na polisi kwa ajili ya kutoa maelezo kuhusiana na kauli aliyoitoa hivi karibuni ambapo kiongozi huyo alinukuliwa akihamasisha maandamano ya wafuasi wa chama chake kupinga kuendelea kwa vikao vya bunge maalumu la katiba.

Awali vurugu hizo zilihusisha wafuasi wa Chadema na askari wa kutuliza ghasia FFU, lakini ghafla zikabadilika na kuwa kati ya polisi na waandishi wa habari, hatua iliyotokana na polisi kuanza kuwapiga waandishi na kuwafukuza kwa kutumia mbwa maalumu, kitendo ambacho kimelalamikiwa na waandishi na hali ilikuwa kama hivi.

Tukio la kupigwa kwa waandishi wa habari, limetokea siku moja baada ya Makamu wa Rais Dkt Mohammed Gharib Bilal, kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama likiwemo jeshi la polisi, kufanya kazi kwa ushirikiano na wanahabari, kutokana na pande zote mbili kuwa na jukumu moja kuu la kuwatumikia Watanzania.

Awali, askari wenye silaha waliwazuia kuingia ndani ya ofisi za makao makuu ya polisi, wabunge kadhaa wa Chadema, akiwemo Mbunge wa Iringa Mjini Mchungaji Peter Msigwa, Mbunge wa Iramba Mashariki Tundu Lissu, Mbunge wa Ubungo John Mnyika na mwenzake wa jimbo la Ilemela Ezekiah Wenje.

Hatua hiyo ilizusha majibizano baina ya pande hizo ambapo wafuasi wa Chadema walikuwa waking'ang'ania wabunge wao waingie ndani kwa madai kuwa baadhi ya wabunge hao wana nyadhifa muhimu ndani ya chama na kwamba ingekuwa vema waingie na kufahamu anachohojiwa Mwenyekiti wao.