Wednesday , 29th May , 2019

Kuelekea Juni 1, 2019, siku ambayo sheria mpya ya Usimamizi wa Mazingira inayopiga marufuku matumizi ya mifuko ya plastiki itaanza kutumika kwa kuwachukulia haua watakaokiuka masharti, hizi ni baadhi ya kanuni za kufahamu.

Vifungashio vya plastiki

Sehemu ya Tatu ya sheria hiyo kwenye kanuni ya tano, inapiga marufuku mifuko hiyo kutumika, kuzalishwa, kuingizwa nchini au kusafirishwa nje ya nchini pamoja na matumizi mengine yoyote ndani ya Tanzania Bara.

Katika kanuni hizo za kupiga marufuku mifuko ya plastiki za mwaka 2019, sehemu ya 4 kanuni ya 9 inatoa ruhusa kwa vifungashio vya plastiki kutumika kwenye matumizi yafuatayo.

''Bila kuathiri masharti ya kanuni ya 5, vifungashio vya plastiki kwaajili ya huduma za afya au bidhaa za viwandani au sekta ya ujenzi au sekta ya kilimo au vyakula au usafi na udhibiti wa taka havitahusika na zuio la kanuni hizi'', imeeleza sehemu hiyo ya kanuni.

Sehemu ya sita ya kanuni hizo inajikita kwenye matumizi mbalimbali ambapo inapiga marufuku mtu yeyote kuuza bidhaa kama vinywaji au bidhaa nyingine zikiwa zimefungwa kwenye vifungashio vya plastiki ispokuwa tu kama bidhaa hizo zinalazimu kutumia vifungashio vya plastiki.