Saturday , 9th Aug , 2014

Rais wa Malawi Peter Mutharika amemualika Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Kikwete kuitembelea nchi hiyo kwa ziara ya kiserikali na kutaka kumalizika kwa mgogoro wa mpaka wa ziwa Nyasa kati ya nchi hizo mbili.

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete.

Kulingana na taarifa iliyotolewa na kurugenzi ya mawasiliano ya ikulu jijini Dar es salaam jana imesema Rais Mutharika amemualika Rais Kikwete kwa dhana ya kuimarisha mahusiano ya nchi hizo mbili na kudumisha udugu. Rais Mutharika ambaye aliapishwa kuwa Rais wa Malawi Mei 30, mwaka huu, alimwalika Rais Kikwete kutembelea Malawi.

Viongozi hao wawili walikutana Georgetown, Washington D.C. nchini Marekani ambako walihudhuria mkutano wa viongozi wa nchi za Marekani na Afrika, uliomalizika juzi.

Wakati wa mazungumzo kati ya viongozi hao jijini Washington,Rais Mutharika amesema kuwa Tanzania ni nyumbani kwake kwani kiongozi huyo amesoma Chuo kikuu cha Dar es salaam hata kabla ya Rais Kikwete hajasoma katika chuo hicho.