Thursday , 1st Nov , 2018

Msanii wa Filamu, Wema Sepetu amesomewa kosa moja la kuchapisha video yake ya picha ya ngono kupitia kurasa yake ya Instagram katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Mwanadada Wema Sepetu.

Wema amesomewa kosa hilo na Wakili wa Serikali Mwanaamina Kombakono mbele ya Hakimu Mkazi, Maila Kasonde.

Wakili Kombakono amedai kuwa mshtakiwa anakabiliwa na kosa moja la kuchapisha picha za ngono kinyume na sheria.

Anadaiwa ametenda kosa hilo, Oktoba 15, 2018 katika sehemu tofauti tofauti ambapo alichapisha kupitia mtandao wake  wa  Instagram video yake ya picha za kingono kitu ambacho hakiruhusiwi.

Baada ya kusomewa kosa hilo, Hakimu Kasonde alimuuliza Wema,

HAKIMU: Mshtakiwa umesikia mashtaka yako ?

WEMA:  Ndio

HAKIMU:  Ni kweli ulichapisha hizo taarifa kupitia Instagram yako ?

WEMA: Sio kweli.

Baada ya kukana wakili wa utetezi, Semwanza Rubeni alimuombea dhamana mteja wake.

Hata hivyo, Wakili wa serikali Kombakono amedai kuwa licha ya dhamana ni haki ya Kikatiba anaiomba mahakama imuwekee masharti magumu kwa sababu Wema anafuatiliwa na idadi kubwa ya watu kupitia mtandao wake wa Instagram ikiwemo watoto.

Katika uamuzi wake, Hakimu Kasonde amesema anatoa masharti ya dhamana ambapo Wema anatakiwa asaini Bondi ya shilingi milioni 10 na awe na mdhamini mmoja atakayesaini kiasi hicho.

Pia amesema anatakiwa asiweke picha yoyote yenye maudhui ya  'Ngono' kwenye mtandao wake wa Instagram wala maneno yenye uelekeo ama viashiria vya kingono.

Wema kaachiwa kwa dhamana, kesi imeahirishwa hadi Novemba 11,2018.