Monday , 17th Sep , 2018

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Tanzania ndio nchi ya kwanza katika bara la Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, kuanzisha vituo vya utoaji wa matibabu kwa waathirika wa dawa za kulevya mwaka 2011.

Bendera ya Tanzania

Waziri Majaliwa ameeleza hayo leo Septemba 17, 2018 baada ya kufungua mkutano wa 28 wa wakuu wa vyombo vinavyopambana na dawa za kulevya kutoka nchi za Afrika ujulikanao kama (28th HONLEA- Afrika), jijini Dar es Salaam ambapo lengo la mkutano huo ni kubadilishana uzoefu na kupanga mikakati ya pamoja kuhusu udhibiti na mapambano dhidi ya biashara ya dawa za kulevya katika nchi hizo.

Aidha, Waziri Majaliwa amesema kuwa hadi kufikia mwishoni mwa 2017, jumla vituo sita vya kutolea matibabu vilianzishwa, ambapo zaidi ya waathirika 6,500 wa dawa za kulevya aina ya heroin walijiandikisha na kupatiwa matibabu.

Mbali na hilo, Waziri Majaliwa amesema matumizi ya dawa za kulevya nchini yamepungua kwa asilimia 90 baada ya serikali kufanikiwa kudhibiti biashara hiyo.

"Ni lazima tuwe na mikakati ya pamoja ya kudhibiti uzalishaji, usambazaji na matumizi ya dawa za kulevya barani Afrika. Hata hivyo ni muhimu kudhibiti njia zote zinazotumika kusafirisha dawa za kulevya", amesema Majaliwa.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema matumizi ya dawa za kulevya nchini yameathiri sekta mbalimbali ikiwemo ya afya, uchumi na jamii, huku uchunguzi ukibainisha kuwa kati ya asimilia 20 hadi 50 ya watumiaji wanamaambuzi ya ugonjwa wa UKIMWI.