Tuesday , 10th Jul , 2018

Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoa wa Kigoma, Amatus Nzamba amesema kuwa kuungana kwa vyama vya upinzani katika uchaguzi mdogo wa jimbo la Buyugu ni dhahiri kwamba vyama hivyo havina wanachama.

Pichani ni Nembo za Vyama vya CHADEMA na ACT-Wazalendo.

Nzamba amefunguka hayo wakati akizungumza na www.eatv.tv, ambapo amedai kuwa kuungana kwa upinzani haiwapi tabu wao kama chama tawala na lazima jimbo hilo lirejee Chama cha Mapinduzi japo lilikuwa likisimamiwa na mbunge wa upinzani marehemu Kasuku Bilago aliyekuwa Mbunge kupitia CHADEMA.

Muunganiko wa CHADEMA na ACT wala haututishi kwanza inaonesha kuwa vyama bado ni vichanga na hawana wanachama ndio maana wameamua kuunganisha nguvu lakini bado haitawasaidia kwakuwa sisi tuna wanachama na wapiga kura”, amesema Nzamba.

Wakiwa kwenye mazishi ya Mwalimu Bilago ambaye alikuwa Mbunge kupitia CHADEMA, Zitto Kabwe pamoja na Mbowe walikubaliana kuweka umoja ambao utamsimamisha mgombea mmoja anayekubalika kutoka upinzani na kuhakikishia wanampigania hadi anashinda ili kumuenzi mwalimu Bilago.

Jimbo la Buyungu limekuwa wazi kutokana na kifo cha aliyekuwa Mbunge wa jimbo hilo, Kasuku Samson Bilago aliyefariki Mei 26 mwaka huu na kupelekea jimbo hilo kuwa wazi hadi sasa.

Kufuatia hali hiyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza tarehe rasmi ya uchaguzi mdogo wa Ubunge katika jimbo la Buyugu pamoja na udiwani katika kata 79 za Tanzania Bara ambapo siku ya uchaguzi huo imepangwa kuwa Agosti 12 mwaka huu.