Baadhi ya washiriki wa michuano ya UMISETA wakitembea wakati wa ufunguzi wa moja ya michuano hiyo iliyopita.
Zaidi ya wanamichezo 300 wa michezo mbalimbali wa shule za sekondari za wilaya ya Kinondoni jijini Dar es Salaam wameanza kutoana jasho wakichuana katika mashindano ya UMISETA mkoa wa kielimu wa Kinondoni yanayofanyika katika viwanja vya shule ya sekondari ya Makongo Jijini Dar es Salaam.
Mlezi wa UMISETA mkoa wa Dar es Salaam Celestine Mwangasi pamoja na mratibu wa michuano hiyo Juma Nchimbi wamesema michezo hiyo itatumika kuteua kikosi cha timu ya wilaya hiyo kitakachoshiriki michuano ya Mkoa.
Wanamichezo hao watachuana katika michezo ya mpira wa miguu kwa jinsia zote [wasichana na wavulana], riadha [mbio], mitupo[ tufe na mkuki], kuruka, mpira wa wavu[ volleyball], mpira wa mikono [handball], mpira wa kikapu kwa jinsia zote pamoja na masuala ya utamaduni na taaluma na mpira wa pete [netball] kwa wasichana.
Michuano hiyo ambayo imekata utepe jana itamalizika siku ya jumapili Mei 22 mwaka huu kwa fainali za michezo yote ambapo pia wataalamu wa ufundi wa UMISETA wilayani Kinondoni watateuwa wachezaji bora watakaounda kikosi cha timu ya wilaya hiyo kitakachoshiriki michuano ya Mkoa dhidi ya Wilaya zingine za Ilala na Temeke.