Monday , 9th Jul , 2018

Inakadiriwa kuwa karibu asilimia moja ya wanaume wote kote duniani huathiriwa na ugonjwa wa mabusha, kwa hapa nchini, tatizo hili ni maarufu sana maeneo ya mwambao wa Pwani ya Bahari ya Hindi, mikoa ya Pwani, Tanga na Dar es salaam.

Pichani kulia ni mtu mwenye ugonjwa wa Mabusha, kushoto ni vifuu vya Nazi.

Tofauti na wengi wanavyodhani kuwa mabusha huwapata wanaume tu, wataalamu wanasema ni ugonjwa wa jinsia zote haubagui kwakuwa mbu anayeeneza ugonjwa huo hachagui kwani hata wanawake huambukizwa ugonjwa huo.

Www.eatv.tv imefanya mahojiano na Daktari kutoka Mpango wa taifa wa kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele, Dkt. Oscar Kaitaba ambapo amesema kuwa ugonjwa wa mabusha umekuwa ukienezwa na mbua ambao chanzo chake kikuu ni vifuu vya nazi na madafu baada ya kutumika na kutupwa ovyo mvua zinaponyesha maji hutuama na kugeuka mazalia ya mbu wanao ambukiza ugonjwa huo. 

Wengi wetu tukimaliza kutumia vifuu vya nazi hatufahamu kama vina madhara matokeo yake vinazagaa na kuzalisha mbu, kifuu kinazalisha mbu anaye ambukiza matende na mabusha kutokana na kugeuka mazalia ya mbu pindi mvua zinapoanza kunyesha”, amesema Dkt. Kaitaba.

Daktari ameongeza kuwa, “Busha linawapata pia wanawake lakini wengi huwa hawajitokezi na nadhani kwa sababu zamani kwa mfano walikuwa wakijifungua kwa wakunga wa jadi ilikuwa rahisi kwao kujificha,  kwa wanawake huwa mashavu ya uke yanavimba kiasi cha kuziba kabisa eneo lote la uke na wakati mwingine uvimbe unapozidi huweza kuziba ile njia ya mkojo na hivyo kusababisha kupata mkojo kwa kiwango kidogo mno”.

Dkt. Kaitaba ameongeza kuwa, dhana iliyojengeka kwa jamii kwamba ulaji wa madafu unasababisha mabusha si kweli bali ugonjwa huo unazalishwa na mbu anayezaliwa kutokana na vifuu vya nazi kutupwa ovyo na kuhifadhi maji, lakini wengi huhusisha ugonjwa huo na imani za kishirikina jamboa ambalo wataalamu wa afya wanalipiga vita. 

Mabusha ni uvimbe kwenye korodani ambao unasababishwa na kujaa kwa maji kwenye moja ya sehemu zinazounda korodani na hutokea pale maji yanayotengenezwa kwenye korodani kua mengi sana kuliko yale yanayo ondolewa.