Tuesday , 9th Jan , 2018

Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Jakaya Kikwete leo amehudhuria mazishi ya mchezaji wa zamani wa Tanzania na klabu ya Yanga Athumani Juma 'Chama' kwenye makaburi ya Kisutu Dar es salaam.

Athumani Juma amefariki dunia jana katika hospitali ya Taifa ya Muhimbili alipokuwa amelazwa kwa matibabu ya ugonjwa wa Kiharusi. Mazishi yake yamefanyika majira ya saa 7:00 mchana.

Katika mazishi hayo yaliyoratibiwa na klabu ya Yanga chini ya katibu mkuu Charles Mkwasa ambaye pia alicheza na marehemu Chama katika kikosi cha Yanga, yamehudhuriwa pia na Waziri wa Mambo ya Ndani Mh. Mwigulu Nchemba.

Dkt. Jakaya Kikwete na Mh. Mwigulu ni wanachama wa muda mrefu wa klabu hiyo. Yanga imewahi kumtumia Mh. Mwigulu katika mambo mbalimbali ikiwemo kumrudisha kazini kocha wa zamani wa timu hiyo Hans Van Pluijm ambaye hivi sasa ni kocha wa Singida United.

Chama alianza maisha ya soka katika timu ya Pamba FC ya Mwanza kabla ya kutua Yanga mwaka 1981. Baadae Chama aliteuliwa kuwa nahodha wa timu ya Yanga na timu ya taifa ya Tanzania. Chama alistaafu soka mwaka 1990.