Monday , 16th Oct , 2017

Wanafunzi watano na mlinzi wa shule wameuawa kwa kupigwa risasi na mwanafunzi mwenzao, huku wengine 17 wakijeruhiwa katika shule ya sekondari ya Lokichogio iliyopo kaunti ya Turkana, nchini Kenya.

Tukio hilo limetokea mwishoni mwa wiki hii ambapo mwanafunzi huyo aliyetambulika kwa jina la Abraham mwenye asili ya SUdan Kusini alikwenda shuleni akiwa na wenzake, na kuanza kuwamiminia risasi wanafunzi ambao walikuwepo kwenye shule hiyo, kwa kinachoaminika kuwa ni kulipiza kisasi baada ya kusimamishwa sule kwa utovu wa nidhamu.

Mashuhuda wa tukio hilo wamesema mwanafunzi huyo alifanikiwa kuingia shuleni hapo baada ya kumuua mlinzi na kisha kuingia bwenini, na kufanya shambulio lililopelekea vifo hivyo na kujeruhi wengine.

Mwalimu mkuu wa shule hiyo amesema kuna ulazima wa kukagua wanafunzi wanaotoka maeneo ya karibu kabla hawajawasajili kwenye shule zao, ili kujiepusha na matukio kama hayo kuendelea kutokea.

Mtuhumiwa huyo ambaye alikuwa mwanafunzi wa kidato cha kwanza alikamatwa na polisi akijaribu kukimbia kuelekea kwenye kambi ya wakimbizi ya SUdan Kusini, na kumpeleka kituo cha polisi, lakini baada ya muda wananchi walivamia kituo hiko na kukishambulia, wakitaka kumuua kwa mawe.

Kufuatia tukio hilo uongozi wa shule hiyo umetangaza kuifunga shule hiyo kwa muda, ili wanafunzi wakae sawa kisaikolojia, kufuatia kile walichokishuhudia.